Monday, November 11, 2013

Kenya yamuunga mkono JK



WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, ameipongeza Tanzania kwa hatua ya kutangaza kuwa haiko tayari kutoka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kama ilivyodhaniwa hapo awali. Akizungumza Dar es Salaam jana, alisema Kenya inaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Novemba 7, mwaka huu kuwa haitajitoa na wala haitakuwa chanzo cha kuvunjika kwa EAC.

Alisema bila Tanzania hakuna Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.

“Kama unavyojua Kenya na Tanzania tumekuwa tukiijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu, tuko na mafanikio mengi, kuna mambo mengi tumeyafanya, kuna njia ndefu imebakia na kuna mambo mengi yasiyoweza kupimwa kati ya nchi hizi.

“Tuna tumaini kwamba tutaendelea kuijenga Afrika Mashariki kwa nguvu zote na tutawasiliana na watu wetu kwa sababu tunataka watu wetu waishi vema na wawe majirani wazuri na tuendelee kuwa hivyo,” alisema Amina.

Amina ambaye ametumwa na Rais Uhuru Kenyata kuja kutoa ujumbe huo, alisema ni vyema nchi hizo zikaendelea kushirikiana kwa kuwa zenyewe ni za kwanza kuunda umoja huo, hivyo ziendelee kuungana kwa ajili ya kuudumisha.

Alisema walikuwa na wasiwasi kuwa Tanzania ingejitoa kutoka EAC, kutokana na hali iliyojitokeza kwa baadhi ya nchi kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha pamoja na Burundi.

Alisema kuwa hakuna namna ambavyo Tanzania na Kenya zitatenganishwa kwa namna ambavyo zimejenga muingiliano mkubwa wa kijamii na kiuchumi, huku akiomba Tanzania kuisaidia kusukuma ombi la Kenya la kutaka kesi inayomkabili Rais Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi kwa ajili ya kumpa fursa ya kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, alisema Serikali yake imefurahi kuona Kenya imekuwa nchi ya kwanza kuipongeza kwa kuinusuru EAC kama ilivyokuwa mwanzoni na kujenga jumuiya ya watu na si ya viongozi.

Aliahidi kushirikiana na Kenya katika masuala mbalimbali likiwamo la kutaka kesi inayomkabili Rais Kenyatta katika mahakama ya ICC iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi.

Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kamwe ushirikiano wa Kenya, Uganda na Rwanda wa kuzitenga Tanzania na Burundi katika mipango ya EAC usingedumu kwa sababu uongozi wao ni wa kidikteta.

Akizungumza Dar es Salaam jana juu ya hotuba ya Rais Kikwete kuhusu EAC, alisema chama hicho kinaunga mkono msimamo wa Tanzania.

Alisema CUF kinalaani vikali vitimbwi vilivyokuwa vikifanywa na Rais wa Rwanda, Kenya na Uganda na kuitenga Tanzania na Burundi na kuongeza kuna haja sasa ya kuwa na tahadhari na viongozi hao katika suala la usalama wa raia na nchi kwa ujumla.

Alisema ushirika wa nchi hizo na mipango yao iliyokuwa ikifanyika isingedumu, kwa sababu uongozi wa Uganda na Rwanda ni wa kidikteta huku Kenya haina umoja wa kitaifa kutokana na kugawanyika vipande viwili.

“Ninachomuomba Rais Kikwete watakapokutana wakuu wa nchi hizo awape vidonge vyao, najua mwezi huu Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano ya mkutano wa 15 kwa wakuu wa nchi,” alisema na kuongeza:

“Tumesikia baada ya hotuba ya Rais Kikwete, wameanza kujing’atang’ata lakini walichokuwa wakifikiria kukifanya ni ndoto za mchana, mfano Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta tangu achaguliwe anasuasua kufanya mikutano upande wa upinzani wake na hilo limeifanya nchi kukosa umoja wa kitaifa.

“Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekuwa mstari wa mbele kuharakisha kufikia Shirikisho la Kisiasa kwa lengo la kutaka kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

“Shirikisho la kisiasa la Kenya, Uganda na Rwanda hizo ni ndoto na wanajifurahisha katika karne hii ya 21, shirikisho lazima lijikite katika mfumo wa demokrasia, Kenya imepiga hatua kubwa kujenga demokrasia lakini haijafanikiwa kujenga umoja wa kitaifa.

“Namuomba Rais Kikwete kuwa makini katika suala la soko la pamoja hasa katika ajira, ardhi na uhamiaji hivyo vitu visiingizwe katika soko la Afrika Mashariki bila kutafakari, Watanzania bado wamezubaa katika ardhi yao.

“Kuna jambo limejificha katika EAC, mimi nadhani ziara ya Rais Barack Obama kuja Tanzania ilielekea kutowafurahisha, ndio maana Kenya ilifikia hatua ya kususia mkutano wa wafanyabiashara wa Afrika ulioandaliwa na Corporate Council on Africa.

“Pia uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda umezorota baada ya Rais Kikwete kuwapa ushauri viongozi wenzake katika mkutano wa Umoja wa Afrika kwamba njia pekee ya kumaliza migogoro ya kisiasa na kuleta amani katika nchi za Kongo, Rwanda na Uganda ni kufanya mazungumzo mezani.

“Jambo jingine ni baada ya Tanzania kukubali kupeleka wanajeshi wake Kongo kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa kuleta amani mashariki ya Kongo, ambapo limesaidia kusambaratisha kundi la waasi wa M23.”

Chanzo: Mtanzania

No comments: