• Yumo
pia mkuu wa majeshi mstaafu
na Abdallah Khamis, Kaliua
WAKATI ripoti ya kamati iliyoundwa na
serikali kuchunguza tuhuma za vigogo walioficha fedha kwenye mabenki ya nje ya
nchi ikiwa bado haijatolewa bungeni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA),
amewataja vigogo watatu kuwa miongoni mwa wahusika.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
wa CHADEMA (Bara), ndiye muasisi wa hoja hiyo bungeni. Hivi karibuni alitishia
kuwataja wahusika endapo serikali haitawasilisha ripoti hiyo kwenye mkutano wa
Bunge uliomalizika Jumamosi.
Mbunge huyo aliwataja vigogo hao juzi
wilayani Kaliua mkoani Tabora wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kolimba.
Bila kutaja majina yao, Zitto
aliwataja kwa nyadhifa zao walizowahi kushika akisema ni aliyewahi kuwa Waziri
wa Nishati na Madini, Waziri wa Ulinzi wa zamani na aliyewahi kuwa mkuu wa
majeshi.
Alisema baada ya kutoa hoja bungeni
ya kuitaka serikali ifanye uchunguzi juu ya Watanzania walioficha fedha nje ya
nchi, alichaguliwa kuongoza timu ya kufuatilia sakata hilo, kupitia taasisi ya
Eurodad, ambapo alifanya ziara katika sehemu mbalimbali ikiwemo nchini Uswisi
na Uingereza.
Zitto alifafanua kuwa akiwa huko
alikutana na wadau mbalimbali wa masuala ya kibenki pamoja na kuhudhuria
mkutano wa Waziri Mkuu wa Uingereza uliokuwa ukizungumzia utoroshwaji wa fedha.
“Hawa watu wanajulikana na tutawataja
kwa majina mchakato ukikamilika, lakini kwa sasa niwaambie miongoni mwa watu
hao ni pamoja na waliowahi kuwa mawaziri na mmoja wa wakuu wa majeshi mstaafu,”
alisema Zitto.
Alisema kutokana na hali hiyo,
serikali inaendelea kushikwa na kigugumizi cha kuwaanika watu hao hadharani
licha ya Serikali ya Uswisi kuitaka isaini mkataba wa kubadilishana taarifa.
Zitto alisema kwa sasa ameshawaagiza
wasaidizi wake katika masuala ya kibunge kuandika utaratibu utakaowasilishwa
bungeni kwa ajili ya kuwadhibiti watu wanaoficha fedha nje bila kuwa na maelezo
ya kutosha.
Aliongeza kuwa suala la kuwaanika
hadharani watu wanaoficha fedha nje ya nchi linahitaji uungwaji mkono wa hali
ya juu kwa kuwa ni kazi ya hatari inayowagusa watu wenye maslahi na uwezo
mkubwa nchini.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, mbali na
Tanzania, nchi nyingi za Afrika zinaweka fedha nyingi Uingereza pamoja na
visiwa vyake 15 ambapo katika kisiwa cha Jersey pekee kuna paundi bilioni 40 za
Uingereza.
Zitto alisema baadhi ya nchi
huwafilisi watu ambao wanabainika kuwa wameficha fedha nje na kuzitumia kwa
shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema kuwa wakati anafanya shughuli
hiyo aliyosema ni ajenda ya kitaifa, alitegemea kuungwa mkono na watu wake wa
karibu, ikiwa ni pamoja na walio ndani ya chama chake.
“Hivi ni vita visivyohitaji utengano,
tunapoamua kulumbana sisi kwa sisi wenzetu wanapata mwanya wa kufanya mambo
yao, nilitegemea katika hali hii CHADEMA tushikamane kuliangamiza hili dude
CCM,” alisema Zitto.
Kuhusu migogoro
Zitto alisema CHADEMA hawama migogoro
na kinachofanyika ni mikakati ya watu wachachahe wasio na shughuli kuamua
kuwagonganisha viongozi.
“Kuna watu wachache sana ambao hawana
kazi, shughuli yao ni kugonganisha viongozi ili wagombane na ikitokea hivyo wao
ndiyo furaha kwao, sio ufahari hata kidogo kwa CHADEMA kuonekana ina migogoro,”
alisema.
Zitto alisema mwaka 1995 kabla ya
CHADEMA kuamua kuiunga mkono NCCR-Mageuzi, Edwin Mtei na Bob Makani waligombea
nafasi ya kutaka kuwania urais kupitia chama hicho na hakukuwa na misigano
yoyote kwa kuwa walijua malengo yao ni kuwatumikia Watanzania.
Aliongeza kuwa hali ya watu kuwania
nafasi moja ndani ya CHADEMA ilijirudia mwaka 1998, kwa nafasi ya uenyekiti
kuwaniwa na watu wawili tofauti na hakukuwa na mgogoro.
“Uchaguzi ndani ya CHADEMA ulifanyika
mwaka 2009, tukapata viongozi na tukaingia kazini, mliona tulichofanya,
tulivuna wabunge wengi, madiwani na wenyeviti wa mitaa. Lakini sasa hali
inaanza kuwa ya ajabu ajabu utafikiri kuna mtu aliyetangaza kugombea,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, hatua yake ya
kugombea uenyekiti mwaka 2009 ilitokana na kile alichokuwa amekiona kuwa
kutekeleza demokrasia ndani ya chama chake kutokana na waliomtangulia
kujitokeza kuwania nafasi walizoona zinawafaa.
“Mimi ni binadamu, nina damu na
nyama, katika umri huu mdogo nimepigwa mishale mingi sana ya kisiasa, ninaumia
na damu inanitoka, sasa nimechoka kupigwa mishale, ni lazima viongozi tuambiane
ukweli na tukemee hali hii,” alisema Zitto.
Alisema kuwa mwanzoni hapakuwa na
chama chenye nguvu kama NCCR-Mageuzi, lakini walipoanza kupigana kile
alichokiita mishale, chama hicho kilisambaratika.
“Wakamchafua sana Mabere Marando kuwa
ndiye msaliti, sasa Marando yuko wapi? Si ni kamanda wetu? Si ndiye huyu
mwanasheria wetu? Lazima tuambiane ukweli na tuweze kuvikwepa vihunzi vya CCM,
lazima sasa wanachama wanaoleta chokochoko washughulikiwe,” alisema.
Alisema kuwa viongozi lazima waonye
haya mambo, kwamba bila kuonya wataonekana wanashiriki.
“Waha tuna msemo; ukiona kifaranga
yupo juu ya chungu, jua mama yake yupo chini,” alisema Zitto.
Kapuya ajisalimisha
Katika hatua nyingine, Mbunge wa
Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), juzi alijisalimisha katika ofisi
ya CHADEMA akimuomba Zitto azungumzie matatizo ya barabara katika jimbo lake
ili aweze kusaidiwa.
Kapuya alitoa ombi hilo katika ofisi
za CHADEMA wilaya baada ya Zitto kuwasili eneo hilo saa 9.30 mchana kwa ajili
ya kufanya mkutano wa hadhara, ikiwa ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati
alipohutubia mkutano wa awali kwa njia ya simu wiki tatu zilizopita.
Akiwa ofisini hapo, Prof. Kapuya
alihojiwa na Zitto akitaka kujua sababu ya kuikodishia Halmashauri ya Kaliua
nyumba yake huku akiwa ni mmoja wa madiwani wa wilaya hiyo wanaopaswa
kuhakikisha halmashauri inakuwa na majengo yake.
“Karibu mzee katika ofisi zetu,
lakini unaweza kuniambia kama uamuzi wako wa kuikodishia halmashauri nyumba
yako hauingiliani na vikwazo vya kuiwezesha kupata majengo yake?” alihoji
Zitto.
Katika kujitetea, Prof. Kapuya
alisema sababu ya kufanya biashara hiyo na halmashauri ni kutokana na wilaya
kutokuwa na majengo yake binafsi.
“Ni kweli mimi ninakodisha, lakini
kiasi ninachochukua ni kidogo kuliko kile anachochukua Waziri Magufuli katika
Wilaya ya Chato, kwani naye anaikodishia halmashauri ya wilaya yake jengo
linalotumika kama ofisi,” alisema Kapuya.
Katika hali ya kuonyesha kuwa anaomba
Zitto asizungumzie upungufu uliopo katika jimbo lake, Prof. Kapuya alimuomba
azungumzie matatizo ya barabara.
Zitto alisema kimaadili kiongozi
anapofanya biashara sehemu anayoweza kuwa na uamuzi inasababisha hali ya
kulinda maslahi ya kiongozi huyo ikiwa ni pamoja na kukwamisha mradi wa eneo
husika usikamilike au kujiongezea gharama katika biashara husika.
Alimueleza Prof. Kapuya kuwa
kinachosabaisha Mkoa wa Tabora usiendelee, ni pamoja na matatizo ya ubinafsi
kati ya wabunge wa mkoa huo, huku akiwaambia waache tofauti zao na Mbunge wa
Urambo Mashariki, Samuel Sitta katika kuwatumikia wananchi.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment