Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (kushoto) akiteta na
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafuli walipohudhuria kikao cha Bunge, mjini
Dodoma jana, Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Waandishi
Wetu, Mwananchi
Shinyanga na Mwanza.Hali ndani ya Chadema inazidi kuwa si
shwari kutokana na migogoro inayozidi kupiga kambi. Safari hii ikiwa katika
Kanda ya Ziwa Mashariki ambako uongozi mzima wa Mkoa wa Mara, umetimuliwa.
Mbunge wa Maswa Magharibi, John
Shibuda, pia amefukuzwa katika kikao baada ya wajumbe kupiga kura ya kutokuwa
na imani naye.
Hatua hizo zimekuja siku kadhaa baada
ya Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kutimuliwa katika
kikao cha Baraza la Kanda ya Kaskazini, kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Katika tukio la Kanda ya Ziwa
Mashariki, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Mara, Bathlomeo Machage, amevuliwa
uongozi na nafasi yake kushikwa na Charles Leyela.
Machage anatuhumiwa kushindwa
kuendesha vikao na kuzorotesha maendeleo ya chama kwa jumla.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumain
Makene, alisema jana kuwa mwenyekiti huyo amesimamishwa kutokana na tuhuma
mbalimbali.
Hata hivyo, tuhuma hizo zilipingwa
vikali na Machage ambaye alisema hatua hiyo dhidi yake ni batili kwa madai kuwa
katiba haivipi mamlaka vikao vya kanda kutimua viongozi.
Alisema yeye bado ni kiongozi halali
wa Chadema mkoani Mara.
Alisema uamuzi huo uliofikiwa katika
kikao cha viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki, ulipaswa kufanywa na Baraza Kuu
la chama.
Alisema Chadema ni chama cha watu
kinachojiendesha kwa misingi ya katiba na kwamba kwa kuzingatia hilo, uamuzi wa
kumwondoa katika uongozi unapaswa kufanywa na Baraza Kuu.Alisema mfumo wa
uongozi wa kanda ulianza hivi karibuni na kwamba kamwe kikao cha kanda hakiwezi
kumfukuza kiongozi wa ngazi ya juu kama yeye.
“Chama kina katiba na kwa mujibu wa
katiba hiyo kiongozi wa chama mkoa ni mtu anayechaguliwa na Baraza Kuu, sasa
naondolewaje na kikao cha kanda wakati kikao cha baraza hakijakaa, sijaitwa
kujieleza wala kusomewa tuhuma zangu,” alieleza Machage.
Alisema tuhuma kwamba ameshindwa
kuitisha vikao, hazina msingi kwa sababu jukumu hilo ni la katibu.
Kwa upande wake, Shibuda alisema
uamuzi wa kumtoa nje, ulikuja baada ya mjumbe mmoja kutoa hoja ya kumtaka
atolewe kwa madai kuwa amekuwa wakihudhuria vikao vya CCM.
Alisema uamuzi huo ulifanyika katika
kikao hicho kilichoketi mkoani Shinyanga chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe.
Mbunge huyo alisema yeye binafsi
amesikitishwa mno na hatua hiyo kwa madai kuwa hajawahi kukisaliti chama.
“Mimi siyo msaliti kwa nilichokifanya
ni kutetea haki na masilahi ya wapiga kura wangu, wakulima na wafugaji. Pale
Meatu nilipanda katika jukwaa la CCM kumweleza katibu mkuu wa chama hicho
matatizo ya wapigakura wangu, maana yeye ndiye mwenye serikali iliyoko
madarakani hivi sasa,” alisema Shibuda.
Mjumbe aliyetoa hoja dhidi ya mbunge
huyo, alikuwa Ahmed Nkunda, kutoka Mwibara.
Kitendo hicho kilisababisha mvutano
mkali uliomlazimisha Mbowe kuwatuliza wajumbe na kuamua kuendesha upigaji kura
za ndiyo na hapana ili kuona wangapi waliokuwa wakiunga mkono hoja na wale
waliokuwa hawaafiki.
Baada ya kuhesabiwa kwa kura za
vidole, wajumbe 90 waliunga mkono hoja na wengi 30 waliipinga. Kwa matokeo hayo
Shibuda aliamriwa kutoka ndani ya ukumbi wa kikao.
Mwenyekiti wa Chadema katika Kanda ya
Ziwa Mashariki, Silvester Nhoja, alisema Shibuda alitolewa kwa matakwa ya
wajumbe baada ya mvutano.
“Shibuda alilalamikiwa na wajumbe
ambao walimtaka atoke nje , Mbowe alilazimika kuwatuliza wajumbe na kuwataka
wampe nafasi Shibuda ajieleze lakini wajumbe waligoma na baadaye zikapigwa
kura, zlizoamua Shibuda kutolewa nje,” alisema.
Mvurugano katika chama hicho
kinachoongozwa kwa upinzani dhidi ya chama tawala, umekuwa mkali katika siku za
hivi karibuni.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment