Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Na Goodluck
Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Suala la tofauti ya ushuru wa
forodha katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, kati ya Zanzibar na Tanzania
Bara, limechukua sura mpya baada ya Serikali kukiri kuwa linaumiza
wafanyabiashara.
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
Salum alisema kuwa tofauti hizo zitaondolewa baada ya sehemu hizo mbili kuanza
kutumia mfumo mmoja wa utozaji kodi na ushuru.
Alisema kuwa utaratibu wa kutumia
mfumo mmoja wa kulipa kodi unatarajiwa kuanza baada ya makubalino, utapunguza
malalamiko ya wafanyabiashara ambao wanadhani hawatendewi haki.
Saada alisema kuwa baadhi ya
wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kulipa kodi mara mbili, wanapokwenda
Zanzibar kununua bidhaa ambapo pia hulazimika kuzilipia tena wanapofika Bandari
ya Dar es Salaam.
Wakati naibu waziri huyo akieleza
hayo, wafanyabiashara wengi wa jijini Dar es Salaam wanalalamika kwamba watu
wanaoingiza bidhaa kupitia Bandari ya Zanzibar wanatozwa kiasi kidogo
ikiliganishwa na wale wanaoingiza kupitia Tanzania Bara..
Walidai kuwa kontena moja la futi 40
hutozwa kodi Sh2.5 milioni Zanzibar wakati kontena kama hilo hutozwa kati ya Sh25
milioni na Sh30 milioni Tanzania Bara.
Shimbe Kinena ambaye ni
mfanyabiashara wa nguo jijini Dar es Salaam alisema kuwa bidhaa zinazoingizwa
nchini kupitia Bandari ya Zanzibar hutozwa
ushuru mdogo na baadaye kuingizwa
jijini kinyemela kwa njia za panya ikiwamo bandari bubu.
Alisema kuwa hali hiyo inawafanya
wanaoingiza bidhaa kutoka nje kupitia bandari na njia za barabara Tanzania Bara
kushindwa kuuza bidhaa, zao kwa vile zile zinazoingia kupitia Zanzibar huuzwa
kwa bei ya chee.
Waziri Saada akizungumzia madai ya
kontena moja la futi 40 kutozwa kodi ya ndogo Zanzibar, ukilinganisha na bara
alisema: “Siwezi kuthibitisha kama gharama ndiyo zipo hivyo, ninachojua kwa
upande wa Zanzibar malipo yanaweza kuwa hata nusu ya yale ya Bara.”
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema kuwa
mfumo mmoja wa ulipaji kodi utaondoa tofauti za viwango vya kulipa kodi
vilivyopo sasa.
Hata hivyo, alikanusha kuwa gharama
za kulipia kontena moja kwa Zanzibar ni ndogo ikilinganishwa na zile za
Tanzania Bara.
“Siyo sahihi kwamba gharama za
kulipia kontena Zanzibar ni ndogo sana kuliko Tanzania Bara kwa sababu
kinachoangaliwa kwenye kontena ni thamani ya mzigo uliopo ndani na siyo kwamba
kuna bei maalumu iliyowekwa,”alisema.
Alisema kwamba kuna viwango maalumu
vya kisheria vilivyowekwa kwa pande zote mbili vinavyofuatwa na kwamba
vitabadilishwa utaratibu mpya utakapoanza.
Alibainisha kuwa mpango huo
unaoratibiwa na Serikali utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa sera
husika.
“Hilo ndiyo lengo letu, ni jambo la
kisera, ambalo sisi tunaletewa na kutekeleza tu…ubishi uliopo sasa kuhusu
tofauti za kodi hautakuwepo,” alisema Kayombo.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment