Moshi. Askari polisi wawili wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU), wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kula njama na kushiriki
katika uporaji wa Sh220 milioni za Kampuni ya Dot Services ya mjini Moshi.
Habari za uhakika zilisema baada ya
kubanwa na makachero, askari hao walirejesha Sh60 milioni na watuhumiwa wengine
wawili ambao ni raia, walirejesha Sh23 milioni. Askari hao ni wale walioko
katika Kikosi cha Polisi wa doria wanaotumia pikipiki na jana watuhumiwa wote
walitawanywa katika vituo mbalimbali ili wahojiwe kwa nyakati tofauti tofauti.
Habari za kipolisi zilisema askari
hao hawakwenda eneo la tukio lakini walifahamu mpango mzima kuhusu uporaji huo
uliowawezesha kupata mgawo wa fedha hizo.
Waliotiwa mbaroni wana vyeo vya
Constable (majina tunayo) na inaelezwa kuwa tukio hilo limewachukiza baadhi ya
polisi wakidai ni kuwa mfululizo wa matukio yanayochafua sura ya jeshi hilo.
Habari hizo zimebainisha kuwa tukio
hilo ni mpango mahususi uliowashirikisha watu wasiopungua 10 wakiwamo baadhi ya
watumishi wa Kampuni ya Dot Services waliovujisha mpango wa kuhamisha fedha
hizo.
Kulingana na vyanzo vya habari, idadi
ya walioshiriki katika mpango wa kupora fedha hizo ni kati ya watu wanane na 10
na tayari polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa
Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa akisema kuwa fedha hizo ziliporwa Jumanne
asubuhi katika makutano ya Barabara za Arusha na Boma mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya
kufika katika makutano hayo, wafanyakazi wa Kampuni ya Dot Services waliokuwa
na gari aina ya Toyota Hilux T.864 AZM walisimama kuruhusu pikipiki ipite.
Kamanda Boaz alisema wakati
wakisubiri pikipiki ipite, ghafla walijitokeza watu wawili wakafungua milango
na kuingia ndani ya gari na kuwateka wafanyakazi na kuwaamuru waelekee eneo la
Shanty Town.
Hata hivyo mkurugenzi wa Fedha wa
kampuni hiyo ya ujenzi yenye makao yake makuu nchini Uganda, Shuresh Bab alifanikiwa
kuruka kwenye gari hilo na kutoa taarifa polisi.
Kamanda Boaz alifafanua kuwa msako wa
kuwatafuta wahusika ulianza mara moja ambapo polisi walifanikiwa kulipata gari
hilo na wafanyakazi wakiwa wametelekezwa mto Karanga mjini Moshi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment