Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa
Jamii, Dk. Seif Rashid (HM)
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kuwasilisha haraka muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa watanzania wote
ikijumuisha makundi maalumu ya wazee, watu maskini na walemavu wasio na uwezo
ili wanufaike na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa
wiki na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi. Jenista Mhagama wakati akifungua semina
ya Bima ya Afya kwa wajumbe wa kamati hiyo mjini Dodoma.
"Sisi kama Kamati tumedhamiria
kwamba Watanzania wote wapate huduma za matibabu kupitia utaratibu huu wa Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya kwani ndio wenye manufaa makubwa kwa wanajamii,"
alisema.
Akitoa maelezo ya utangulizi katika
Semina hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa
tayari ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Mfuko kuandaa mapendekezo hayo ili
kuhakikisha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya unaandaliwa haraka na
kuwasilishwa kwa Serikali haraka iwezekanavyo.
Naye Mbunge wa Viti maalumu Bi.
Hokololo ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Mfuko kwa hatua na kazi nzuri
inayofanya katika kutekeleza majukumu yake. Alisema sasa ni muda muafaka kwa
menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuangalia upya suala la uhaba wa
dawa kwa kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa.
Akichangia mada, Mbunge wa Arusha
Mjini Godbless Lema, ameupongeza Mfuko huo kwa kazi nzuri lakini ametoa
angalizo kwamba juhudi zinazofanywa na Mfuko huo hazitakuwa na maana kama
Watumishi wa Sekta ya Afya hawatakuwa na utu kwa wagongwa wakati wa kutoa
huduma.
Aidha ameishauri serikali kuangalia
upya namna ya kuboresha motisha kwa watumishi katika sekta ya afya.
Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa
Jamii, Dk. Seif Rashid kitoa ufafanuzi wa hoja za ujumla za kisera na hasa
kuhusu changamoto ya uhaba wa dawa na utendaji wa Bohari Kuu ya Serikali Dawa
(MSD) imeiambia Kamati hiyo kwamba kuanzia sasa Dawa zote zitawekwa alama
maalumu ya Serikali ili kuwabaini wale wote wanaohujumu juhudi za Serikali na
kwa sasa Serikali imekwisha kamilisha mchakato wa kuimarisha Mfumo mzima wa
utendaji wa MSD kupitia kwa mkandarasi mshauri aliyepewa kazi hiyo.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za
wabunge, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Hamisi Mdee amesema tatizo
kubwa lililopo katika ufanisi wa utekelezaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii katika
Halmashauri ni kutegemea uongozi wa Mkoa, Halmshauri na Watendaji.
" Ukiona Mfuko wa Afya ya Jamii
unafanya vizuri basi ujue hizo ni juhudi binafsi za viongozi wa ngazi ya Mkoa
na Wilaya kama Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa au Wakurugenzi wa Halmashauri na
wanapohamishwa tu maeneo hayo kila kitu hurudi nyuma," alisema.
Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo, amesema
Mfuko wa Bima ya Afya ambao kwa sasa unasimamia Mfuko wa Afya ya Jamii kwa
kutoa ushauri wa Kitaalam unamkakati wa kuongeza wigo wa huduma za CHF ili
zipatikane hadi katika ngazi ya hospitali za rufaa ngazi ya Mkoa.
" Hii itawavutia wanajamii walio
wengi kujiunga na taratibu hizi za bima maana atakuwa na uhakika wa kupata
huduma hadi ngazi ya juu badala ya utaratibu ulivyo sasa'' amesema bwana Mdee.
Chanzo:
Mjengwablog
No comments:
Post a Comment