Tuesday, November 12, 2013

IRAN YASISITIZA URANI ITARUTUBISHWA



Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema haki za nchi hiyo za kurutubisha madini ya urani ni mistari mekundu ambayo haiwezi kuvukwa.
Pia amesema Jamhuri hiyo ya Kiislamu ilitumia busara wakati wa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo hivi karibuni.

Akizungumza katika Bunge la taifa hilo jana, Rais huyo alisema wamewaeleza wajumbe wanaozungumza nao kuhusu mpango huo wa nyuklia kwamba hawatosalimu amri kwa vitisho vyovyote vile, vikwazo, hila au kwa kubaguliwa na kwamba nchi hiyo haikuinamisha na haitoinamisha kichwa chake kutokana na vitisho kutoka mamlaka yoyote ile.

Alisema kwamba, kuna mistari mekundu ambayo haiwezi kuvukwa na masilahi ya taifa ni mistari mekundu yenye kujumuisha haki chini ya mifumo ya sheria za kimataifa na kurutubisha urani.
Hata hivyo, juzi mataifa sita yenye nguvu duniani yalishindwa kufikia makubaliano ya kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran.

Aidha, yalidai tofauti zao zimepunguwa na wataanza tena mazungumzo katika kipindi cha siku 10 kujaribu kuumaliza mzozo huo uliodumu kwa muongo mmoja.

No comments: