Monday, November 4, 2013

Zitto, Lema waparurana



POSHO za vikao zimezidi kuwagawa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini). Kuwagawa huko kumekuja baada ya Lema kupitia taarifa yake aliyoituma katika mtandao wa kijamii jana, kumwita Zitto ni mnafiki.

Katika taarifa hiyo aliyoithibitisha kwa RAI Jumatatu kuwa ni yake, alisema aliposema ni mnafiki kuhusu suala la posho alikuwa na maana kwamba sio kweli kuwa kukataa posho ni uzalendo na hata ingekuwa ni uzalendo Zitto sio mzalendo katika suala hilo na maisha yake.

“Aliposema hatochukua posho wananchi wengi walimuona ni shujaa, ushujaa ambao hana katika jambo hili. Nasema hivi kwa sababu wakati Zitto anakataa posho ya kikao ya shilingi elfu sabini (70,000/-) kwa siku ambayo ni sawa na shilingi takriban milioni kumi na mbili kwa vikao vyote vya Bunge kwa mwaka, anapokea posho ya kikao kati ya shilingi laki saba hadi milioni moja kwa kikao kimoja katika vikao vinavyofanywa na mashirika mbalimbali hususani ya hifadhi za jamii,” alisema Lema na kuongeza:

“Maana yake ni kama anapokea shilingi laki saba kwa siku na mashirika haya kwa ujumla wake yakafanya vikao ishirini tu kwa mwaka na mara nyingi Zitto kama Mwenyekiti wa PAC huwa anapata mwaliko wa kuhudhuria vikao hivi.

“Basi atakuwa akipata posho ya kikao takriban shilingi milioni kumi na nne hadi milioni ishirini kwa vikao visivyozidi ishirini, wakati kule juu amekataa posho ya shilingi milioni takriban kumi na mbili kwa vikao vya siku takriban mia moja na themanini ambayo ni miezi sita.”

Alisema ikiwa vikao hivyo vya mashirika anayohudhuria Zitto kama Mwenyekiti wa PAC ni vya siku 180 kama ilivyo kwa vikao vya Bunge, basi atakuwa anapokea posho kati ya ya Sh 126,600,000 na Sh 180,000,000.

“Hapa naomba kutaja maslahi yangu katika hili, kwani wabunge wa kawaida ikiwa wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa shilingi laki tano kwa kikao kwa siku.

“Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana. Tofauti na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC yeye pamoja na posho anayochukua (Sh 700,000 – Sh 1,000,000) hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege ya kumtoa alipo na kumrudisha na kukodiwa hoteli yenye hadhi ya nyota nne hadi tano kwa siku. Hoteli hiyo hulipiwa kati ya Dola 100-600 za Marekani kwa siku,” alisema Lema.

Alihoji Zitto anayepinga posho ya Sh 70,000 ya kikao cha Bunge ambayo msingi wake ni uwakilishi wa wananchi na kukumbatia posho ya mashirika ambayo msingi wake pengine ni kuwaziba midomo wenyeviti wa Kamati za Bunge ndio uzalendo.

Alisema Zitto anatoka jimbo lenye umasikini mkubwa, ambapo anaamini kuna wahitaji wengi kama yatima, wajane, wazee na wasiojiweza kwa namna mbalimbali.

“Sasa kama yeye ni mzalendo kwanini asingetumia malipo yake hayo halali kuwasaidia hao ndugu, jamaa na wapiga kura wake,” alisema Lema.

“Nina wasiwasi na uzalendo anaouhubiri Zitto na amepoteza mwelekeo wa hoja ya msingi ya Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Chadema juu ya fikra sahihi ya kubadilisha mfumo wa kibadhirifu uliojificha katika posho zisizokuwa na msingi na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kupitia mishahara yao.

Aidha, alitoa msimamo wake kuwa umasikini sio uzalendo na anauchukia umasikini.

“Sipendi umasikini, nachukia umasikini lakini pia sipendi kuona mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka, lakini siwezi pia kukumbatia umasikini kwa lengo la kuthibitisha uzalendo wangu.

“Najua watu wa jimbo langu wanataka maji, umeme na huduma bora za afya na mambo mengi yenye sura hii lakini sitang’oa bomba la maji nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nitamsaidia kwa kadri nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji.

“Julai, 2012, Zitto stahili za mbunge ziliongezwa kwa takriban shilingi milioni tatu ambazo ni sawa na milioni 36 kwa mwaka, je, kwanini Zitto hakugoma kupokea fedha hizo kuonyesha uzalendo wake,” alisema Lema.

Alisema kuna wakati Zitto aliumwa akapelekwa India kutibiwa sasa kwanini hakuwa mzalendo na kufanya mgomo atibiwe hapa nchini kuonyesha uzalendo wake na kuokoa fedha ya Serikali.

“Zitto ningemuelewa kama maisha anayoishi yangeendana na kauli zake za Kikomunisti, lakini maisha yake na matendo yake na mienendo yake yanashindwa kutafsiri kauli zake,” alisema Lema.

Katika kuonyesha kumjibu Lema, Zitto kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook alisema mwaka 2009 akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alikuta utamaduni wa mashirika ya umma/taasisi za Serikali kuwalipa wabunge wanapoitwa katika kamati.

“Niliwashitaki wabunge PCCB kwa matumizi mabaya ya madaraka na kujilipa posho ambazo hawastahili maana Bunge linakuwa limelipa. PCCB wakazuiwa uchunguzi wao na Spika Sitta, hata hivyo utamaduni huo ulikufa na siku hizi hakuna kitu kinachoitwa Parliamentary Expenses katika hesabu za mashirika yote ya umma.

“PAC ilipiga marufuku taasisi za Serikali au mashirika ya umma kulipa wabunge kwa kazi za kibunge. Hivyo hakuna hata mjumbe mmoja wa PAC anayelipwa posho na taasisi yoyote ya Serikali kwa kazi za kibunge,” alisema Zitto.

Alisema wajumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wanalipwa posho kama kamati nyingine.

“Posho za vikao mimi sichukui maana nimezikataa bungeni, nimezikataa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, nimezikataa Baraza la Ushauri la Mkoa wa Kigoma. Hata nikialikwa na NGOs kwa kazi zangu za ubunge sichukui posho yoyote. ‘It is a matter of principle!’

“Sipendi hata kidogo kulumbana na wabunge wenzangu kuhusu suala hili. Ni jambo la hiari ya mtu kuchukua au kutochukua posho. Hebu tujielekeze kutatua kero za wananchi badala ya kulumbana kunakosababisha tutunge uongo ili tu kulilia posho. Mbunge anayelilia posho hastahili kuwa mbunge. Akatafute kazi nyingine,” alisema Zitto.
Chanzo: Mtanzania

No comments: