Monday, November 4, 2013

Membe azionya Uganda, Kenya



WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema muungano ulioanzishwa na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda, ni wa woga. Kutokana na hali hiyo, amesema Tanzania haiwezi kushiriki muungano huo kwa kuwa umejaa ubaguzi unaozitenga baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Membe aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha runinga cha Channel Ten.

Kwa mujibu wa Membe, kitendo cha nchi hizo kuanzisha ushirikiano, kimedhihirisha bila shaka kwamba Kenya, Uganda na Rwanda, hazitaki kuendelea kushirikiana na Tanzania.

“Huu ni muungano wa watu wenye woga, kwa sababu hawawezi kuwa na muungano na kuitenga Tanzania ambayo kimsingi ndiyo mama wa EAC.

“Mhimili mkubwa wa EAC ni Tanzania, kwani hata ukiangalia rasilimali tulizonazo, wingi wa watu, ukiangalia uanachama wetu kwenye nchi 14 za SADC, huwezi kabisa ukasema eti unaitenga Tanzania.

“Lakini, wote huo ni wasiwasi na woga, ni woga gani huo, mimi siujui ingawa pia inawezekana kuna mtu anautaka urais wa EAC sasa anaona Tanzania ndiyo kikwazo au tatizo inawezekana ni ardhi,” alisema Membe.

Pamoja na hayo, alisema kitendo cha nchi hizo kuanzisha muungano, kinadhoofisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa wafanyakazi wa sekretarieti Makao Makuu ya EAC, yaliyoko Arusha, wanapoambiwa wakahudhurie vikao vya nchi hizo tatu vinavyofanyika Kigali, Rwanda, wanajiuliza waende kama wao au watumie mfuko wa EAC.

“Watu wamechanganyikiwa, kwani kama wataamua kutumia mfuko wa EAC wakati mmoja wa wanajumuiya hahusiki, watakuwa wakikiuka taratibu kwani watakayoyafanya hayatalingana na kanuni za jumuiya yetu.

“Lakini pia, hawa wenzetu wanapoutengeneza muungano wao kisha wanaalika nchi nyingine zijiunge nao, hawazitendei nchi hizo haki kwani zilitakiwa kwanza zisajiliwe kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

“Jamani, hakuna jambo linalozihusu Kenya na Uganda halafu lisiihusu Tanzania kwani hata tulipofungua barabara ya kutoka Arusha kwenda Kenya kupitia Namanga, tuliwaita Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi yaani hatukuacha mtu.

“Sasa haya ya kusema mkiwa na jambo kama barabara inazozihusu Uganda, Kenya na Rwanda, wao ndio wakusanyike na wengine hawahusiki, maana ya jumuiya ni nini,” alisema Membe.

Katika mazungumzo yake, Membe alisema Tanzania iko mahali ambapo haiwezi kunyanyasika na kufadhaishwa kwa kuwa inaweza kuhitajiwa na nchi yoyote kwa ajili ya ushirikiano.

“Chombo ambacho kingeweza kusema hakituhitaji, labda kingekuwa ni SADC, lakini hata nao wanasema hapana kwa sababu sisi ni muhimili mkubwa sana,” alisema.

Membe aliwatoa hofu Watanzania kwa kusema hata kama Tanzania itatengwa, hatutaweza kuathirika kwani biashara kwa nchi hizo bado itaendelea kama kawaida.

“Bwana mtu asikudanganye, katika Bara la Afrika, Tanzania ndiyo mfano wa kuigwa ambao wana uzoefu wa masuala ya muungano, sisi tunajua changamoto za muungano, hakuna mtu wa kutuburuza.

“Watanzania wanajua muungano wao na Zanzibar jinsi walivyoulea tangu uhuru hadi sasa, Tanzania inaelewa namna ya kwenda pole pole katika kuunda muungano ulio imara na bora zaidi kuliko wengine wote, suala la muungano siyo la kusema kesho tuwe na sarafu moja, keshokutwa tuunde Serikali moja halafu tuendelee.

“Hakuna kitu duniani kama hicho, kwani hata EU (Jumuiya ya Ulaya) yenyewe Waingereza walikataa kujiunga na Euro badala yake wanaendelea kutumia Paundi yao.

“Federation si harusi ya kukimbilia, mnaweza kupeana talaka ya haraka sana, hapa tulipofikia kwenye soko la pamoja kwa kuruhusu mambo kufanyika kwa bidhaa kwenda kwenye soko lolote la EAC bila ushuru na tukaruhusu wafanyakazi kama walimu na madaktari kwenda kufanya kazi katika nchi hizo, lilikuwa jambo zuri,” alisema Membe.
Chanzo: Mtanzania

No comments: