Waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema
wamesalimu amri baada ya kukabiliwa na mashambulizi makali na jeshi la serikali
linalosaidiwa na Umoja wa Mataifa ili kuwaondoa katika eneo mashariki mwa nchi
hiyo
Kundi
hilo la waasi limesema katika taarifa yake kuwa "limeamua kuanzia leo
kumaliza uasi wake" na badala yake litatimiza malengo yake "kupitia
njia za kisiasa pekee". Hatua hiyo inamaliza uasi ambao umedumu miezi 18
na kuliharibu eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa raslimali na maliasili,
lililokuwa kitovu cha mojawapo ya migogoro mibaya zaidi barani Afrika katika
kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Awali, serikali mjini Kinshasa ilidai
"ushindi kamili" dhidi ya M23 baada ya kuyakomboa maeneo mawili ya
milima yaliyokuwa yametwaliwa na wapiganaji hao.
Lambert Mende, waziri wa mawasiliano
na msemaji wa serikali, amesema "wapiganaji wa mwisho wa M23 wameondoka
katika ngome zao", akiongeza kuwa sasa "waasi hao wamekimbilia
Rwanda."
Naye Luteni Kanali Olivier Amuli,
msemaji wa jeshi katika eneo la Kivu ya Kaskazini ambaye alikuwa katika eneo la
mapigano amesema "tumemaliza kazi". Amuli ameongeza kuwa kabla ya
kutoroka, waasi hao walichoma moto na kuziangamiza kabisa silaha zao, vifaa na
magari waliyokuwa wamepora wakati wakiudhibiti mji wa Goma.
Jeshi la Congo lilisaidiwa na MONUSCO
Jeshi la Congo lilianzisha mapingano
makubwa dhidi ya waasi mnamo tarehe 25 Oktoba, na kwa haraka sana likaweza
kuzikomboa ngome zao hadi pale waasi mwishoni mwa wiki iliyopita walipoelekea
hadi maeneo matatu ya juu ya milima takribani kilomita 80 kaskazini mwa mji
mkuu wa eneo hilo, Goma, na karibu na mpaka wa Rwanda.
Picha ya kutokea angani ya Ziwa Kivu na mji wa Goma, katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini mashariki ya Congo
Waasi hao waliozidiwa nguvu
walisalimu amri, lakini jeshi likaendelea na mashambulizi yao, na kutwaa
mojawapo ya eneo moja la juu yam lima Jumatatu.
Jeshi Maalum la Umoja wa Mataifa
nchini Kongo (MONUSCO), ambalo limekuwa likiwasaidia wanajeshi wa Kongo kwa
kufanya uchunguzi wa angani, ujasusi na mipango, lilijiunga katika uwanja wa
mapambano Jumatatu usiku baada ya kupata idhini ya kuziripua ngome zilizosalia
za waasi. Chanzo cha habari kutoka Kikosi hicho cha MONUSCO kimesema
"wataendelea kuvurumisha mabomu na kufyatua risasi hadi kila kitu
kitakapodhibitiwa."
Safisha safisha yaendelea
Operesheni za safisha safisha bado
zinaendelea, ili kuhakikisha kwamba hamna mpiganaji yeyote wa M23 aliye na
silaha mkononi katika maeneo yote ya wilaya ya Rutshuru, walikokuwa wakiendesha
harakati zao. Siku ya Jumapili, kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa, alitangaza
kuweka chini silaha ili kutoa nafasi ya kuanzishwa tena mazungumzo. Lakini
mapigano yalionekana tu kuongezeka, hata baada ya ombi hilo la kiongozi wa M23,
licha ya taarifa iliyotolewa mapema Jumatatu na wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya,
Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa iliyosema kuwa "wana wasiwasi kuhusu
machafuko yaliyoanzishwa upya" ambayo yalifuatia amri hiyo ya kusitisha
mapingano.
Kwa miongo mingi, eneo la Kivu ya Kaskazini
na Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa kitovu cha mzozo kwa
sababu linazingirwa na mipaka ya Rwanda, Uganda, Burundi na Tanzania, pamoja na
madini yanayopatikana kwa wingi katika milima ya eneo hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/John
Kanyunyu/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo:
DWSwahili
No comments:
Post a Comment