Dar es Salaam. Siku moja baada ya wabunge kuwataka
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki
kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, pembe 706 za
ndovu zimekamatwa jijini Dar es Salaam.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353
waliouawa katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali hapa nchini. Tukio hilo
lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni,
liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe
za ndovu ni raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin
wote kutoka mji wa Guandung .
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi
katika nyumba hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini
vitunguu swaumu kutoka China na kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana
baharini.
Alipoingia ndani ya nyumba hiyo,
Kagasheki ambaye aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa usalama
alishuhudia shehena kubwa ya pembe za ndovu ikiwa imehifadhiwa kwenye viroba
vyenye uzito wa kilo 50.
Mbali ya kushuhudia shehena ya pembe
hizo, alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa hao
hulitumia kutoa pembe porini na kuyaingiza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio mara
baada ya kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na matokeo ya
Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzi baada ya
wabunge kuilalamikia.
Waziri Kagasheki alisema kwamba
katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni kwa
ajili ya kujaribu kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari ili
wasikamatwe,” alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu
kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na
mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete
pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa
rahisi anayeweza kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na
baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya
kisiasa.
“Itakuwa ni jambo la ajabu kwamba
kila mtu akiingia madarakani wanataka atoke, watatolewa wangapi?” alihoji na
kuongeza kuwa operesheni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo wasiishe.
Alisema kwamba ni kweli kuna baadhi
ya dosari zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi ya mifugo,
lakini siyo kwamba zoezi zima halina manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya
kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa
wameisha nchini.
Alisema hataki kuona utawala wa Rais
Kikwete ukiondoka madarakani ukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize
tembo.
Mmoja wa watuhumiwa hao, Huang Qin
alisema shehena yote ya pembe za ndovu iliyokamatwa nyumbani kwake ilikuwa
ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema:
“Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (pembe) kidogo
kidogo.”
Januari mwaka huu, Gazeti La Daily
Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya
vipande 638 vya pembe za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa
kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tani
nne za pembe za ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni sawa na
takriban Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku
ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja
wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa
Vietnam akiwa na pembe za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni
yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment