• Wajipambanua
katika makundi sita ya masilahi
na Mwandishi wetu
SIKU chache baada ya serikali
kusitisha Opereshini Tokomeza Ujangili kutokana na wabunge kuilalamikia wakidai
inakiuka haki za binadamu na mifugo mingi imeuawa, siri imefichuka kwamba
baadhi ya wabunge na vingozi wa serikali wanatumiwa na majangili kudhoofisha
vita dhidi ya ujangili.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka
bungeni na serikalini, majangili hao wamegawanyika katika makundi sita. Wamo
wafugaji, wakulima, watalii, wamiliki wa vitalu vya uwindaji, wabunge, na
viongozi wa serikali ambao wameibuka na kuingilia kati baada ya kuhisi kwamba
wanakaribia kukamatwa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa zaidi
ya sh milioni 200 zimechangwa na majangili hao kwa ajili ya kufanikisha mkakati
wa kuzima opereshini hiyo.
Baadhi ya wabunge wanatumiwa bila
kujua, huku wengine wakifanya hivyo kwa hiari na makusudi ya kunusuru majangili.
Tayari kuna mpasuko mkubwa serikalini
na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na baadhi ya watendaji kubaini
mbinu chafu za kutaka kuzima operesheni hiyo ili kuwanufaisha vinara wa
ujangili.
“Hawa watu wana mtandao mkubwa, baada
ya kubaini wanakaribia kunaswa, sasa wameingia bungeni kwa kuwatumia baadhi ya
wabunge ili waipinge operesheni hiyo,” kilisema chanzo.
Taarifa za uhakika kutoka serikalini
zinasema kuwa majangili hao wamekuwa na jeuri kutokana na kuwazunguka viongozi
wa chini na kuwasiliana moja kwa moja na kigogo, ambaye bila kujua amekuwa
akizunguka viongozi wa wizara, na kukingia kifua majangili.
Baadhi ya vyanzo hivyo vilieleza
kushangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge kutetea uhai wa ng’ombe na kushindwa
kulinda uhai wa tembo wanaouawa na kung’olewa pembe.
Mwishoni mwa wiki, Bunge liliazimia
kuunda kamati teule ili kuchunguza suala hilo huku Waziri Mkuu na mawaziri
wanne wakisulubiwa kwa madai kuwa wameshindwa kuwajibika ipasavyo.
Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel
Nchimbi (Mambo ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo
David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa).
Hata hivyo, gazeti hili limedokezwa
kuwa kwa vyovyote iwavyo serikali haitakuwa tayari kukubali kamati teule hiyo
iundwe kwani ripoti yake inaweza kumng’oa Pinda na hivyo serikali kuanguka.
“Kinachofanyika sasa ni kuletwa kwa
taarifa ya dharura bungeni ya kuonyesha serikali inapendekeza njia mbadala ya
kushughulikia suala hilo ili badala ya kamati teule, iundwe tume huru
itakayoongozwa na jaji kama ambayo CHADEMA wamekuwa wakipendekeza muda mrefu.
“Vita hii ya ujangili ni pana,
imeingia hadi kwenye siasa za makundi ya urais ndani ya CCM, na hivyo kundi
moja linataka kumng’oa Makinda kwenye uspika kwa hofu kuwa anawasikiliza sana
wabunge na mawaziri wa kundi jingine,” kilisema chanzo hicho.
Kwamba Oparesheni Tokomeza Ujangili
inapingwa baada ya vinara hao kubaini wanakaribia kunaswa, na sasa wanataka
kuvuruga ili kazi hiyo irudi nyuma na hata ikiendelea basi wako radhi kutajana
kwa majina kwani miongoni mwao wamo pia wabunge na viongozi wengine.
“Hawa majangili wana jeuri, wao
wanazungumza kwa simu moja kwa moja na mmoja wa vigogo wa ngazi za juu
serikalini, na huko wanasikilizwa. Serikali nayo inajua kuwa operesheni
ikisimama tembo wanakwisha na vile vile kamati teule wakiikubali serikali
inaanguka,” kinasisitiza chanzo.
Vyanzo hivyo vinaainisha kuwa hata
mchakato wa kutaka kumwondoa Makinda kwenye uspika ambao ulikuwa umeanza
kupitia kwa Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla kukusanya kura za wabunge
uliingiliwa na majangili hao.
Vyanzo vya habari vinasema hoja ya
Kigwangalla inasukumwa na wakubwa kadhaa mashabiki wa mmoja wa mawaziri
waandamizi wanaotajwa kutaka kugombea urais 2015, ambao wanaona Makinda
anapendelea wabunge wanaoshabikia kambi ya kigogo mwingine anayesemekana kutaka
urais kwa udi na uvumba.
Habari zinasema kundi la waziri huyo
linaungwa mkono na kigogo mmoja mwandamizi ambaye hataki kabisa kuruhusu
swahiba wake wa zamani agombee urais; na sasa wamedhamiria kumwangusha Makinda.
Hata hivyo, kabla hoja yao haijashika
kasi, wakati wakiendelea kukusanya sahihi za kutosha kumwondoa Makinda,
majangili nao wakapata upenyo kwa kuathiri mwelekeo wa Bunge, na Makinda
anaruhusu mjadala wa ujangili, ambao iwapo kamati teule itaundwa na kufanya
kazi yake barabara, serikali inaweza kuangushwa kabla ya spika huyo kuondolewa.
“Hoja ya Makinda imezimwa, sasa
wabunge wanazungumzia operesheni ya ujangili. Hapa wanajua kuwa spika hawezi
kukubali hoja hiyo iendelee, hivyo naye ataipa kipaumbele kamati teule ili
kuonyesha serikalini kuna tatizo.
“Wanajua hawawezi kumfukuza spika
katika kikao hiki, lakini wakati huo Kamati ya Bunge itakuwa imekamilisha
mchakato na kutoa uamuzi dhidi ya Pinda na mawaziri wenzake, jambo ambalo
linaweza kumnusuru Makinda na kuiangusha serikali,” kilisema chanzo chetu.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM),
ndiye alitaka Bunge lijadili kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji
wengine wa ardhi, huku Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), akitaka Bunge
lijadili vitendo vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Lugola alidai watendaji wamekuwa
wakiwaua kwa risasi ng’ombe waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na
kuwatesa wamiliki wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa
fursa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Mathayo, kuelezea Operesheni Tokomeza Ujangili na migogoro
kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza
kueleza operesheni hiyo inaendelea. Alisema inalenga kutokomeza ujangili
ulioshamiri hapa nchini kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.
Hata hivyo, Kagasheki alisema
kutokana na malalamiko ya watu mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo,
serikali imeamua kuisitisha ili kufanya tathmini.
Waziri huyo pia alisema mifugo yote
iliyokamatwa ndani ya hifadhi kabla na baada ya operesheni hiyo iachiliwe bila
gharama yoyote na watu wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi
wawasilishe vielelezo ili achukue hatua zaidi.
Waziri Mathayo alitoa taarifa kuhusu
migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Aliwaomba radhi waliopata hasara ya
kujeruhiwa, kupoteza mifugo au vifo katika operesheni hiyo.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment