na Happiness Katabazi
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Dk. Sengondo Mvungi (61), amevamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa
kwa mapanga sehemu za kichwani na usoni.
Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria
maafuru nchini na mwanachama wa NCCR-Mageuzi, alivamiwa na watu wanaosadikiwa
kuwa majambazi saa 6:30 usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Kibamba, Kata ya
Mpiji Majohe.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana nje ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa Dk. Mvungi kwa
matibabu, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema watu hao kabla ya
kuvunja milango ya nyumba walilipua kitu ambacho kilitoa moshi mwingi na
cheche kisha kuingia ndani na kuanza kudai wapewe fedha.
Alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha
Dk. Mvungi kupambana nao bila mafanikio, ndipo wakamjeruhi vibaya kwa
kumcharanga mapanga kichwani, usoni na kisha kuondoka na kompyuta mpakato
(Laptop) yake, pisto na kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana.
Mbatia alisema majirani na ndugu
walifanikiwa kumbeba Dk. Mvungi na kumkimbiza katika Hospitali ya Tumbi mkoani
Pwani ambako alipatiwa matibabu ya awali na kisha kuhamishiwa Muhimbili saa
10:00 alfajiri.
Alisema kuwa alipokelewa na kuingizwa
katika wodi ya huduma ya dharura na ilipofika saa 4:16 asubuhi gazeti hili
lilishuhudi Dk. Mvungi ambaye alikuwa hajitambui akitolewa kwenye chumba
hicho na kuingizwa kwenye gari la wagonjwa lenye namba za usajili STK 8767.
Wakati huo, Dk. Mvungi alikuwa
akipelekwa katika Hospitali ya Aghakan kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha
siti scan kwa ajili ya kuona ameathiriwa vipi katika eneo la kichwa.
Mbatia aliongeza kuwa ndugu na
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walifikia uamuzi wa kumpeleka Dk.
Mvungi akapimwe kipimo hicho Aghakan na kisha arejeshwe kwa sababu uongozi wa
MOI uliwaeleza kuwa mtaalamu anayefahamu kutumia kipimo hicho hakuweza
kupatikana mara moja.
Majira ya saa 5:58, Dk. Mvungi
alirejeshwa MOI huku akiwa bado anavuja damu maeneo ya puani na
kichwani na kisha akaingizwa tena katika chumba cha huduma ya dharura.
Baadaye saa nane mchana alihamishwa
katika chumba hicho na kupelekwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalumu (ICU).
“Jamani Watanzania, Dk. Mvungi hali
yake ni mbaya kama mlivyomuona, kwani tangu alivyopigwa jana saa sita usiku
hadi sasa bado anavuja damu…tumeumizwa sana na kitendo hiki na tunaamini
serikali inafanya kazi yake ya kubaini ni wakina nani wamefanya unyama huu,”
alisema Mbatia.
Shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni
dereva wa Dk. Mvungi, alisema kuwa wahalifu hao walikuwa wakisema wanahitaji
fedha ila walimpiga sana na mapanga na kwamba ndiye aliyembeba kumkimbiza Tumbi
na baadaye Muhimbili.
Mke wa Dk. Mvungi, Anna Mvungi,
alisema watu hao walipoingia ndani walitembeza mapanga huku wakimtaka
asiwatazame usoni.
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba waliofika kumjulia hali Dk. Mvungi ni pamoja na Prof. Paramaganda
Kabudi, Joseph Butiku na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Prof. Costa
Mahalu na wahadhiri wengine.
Chanzo:
BBCSwahili
No comments:
Post a Comment