na Edna Bondo
WATANZANIA wametakiwa kuacha mazoea
ya kutegemea ajira serikalini, badala yake wawe wabunifu kwa kujiajiri.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam
jana na Mawakala wa M-Pesa Dar es Salaam na Morogoro walipokuwa wakikabidhiwa
fedha taslimu na vyeti kutoka Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania
ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao.
“Vijana wengi wamekuwa na fikra
tegemezi, wamekuwa watu wa kusubiri serikali iwapatie ajira huku wakijua kabisa
kuwa fursa za ajira katika ofisi za serikali au sekta binafsi ni chache kuliko
nafasi za kujiajiri,” alisema Ziadi Kamanya anayefanya kazi zake Buguruni
sokoni.
Juma Nyange, mkazi wa Tabata alisema
Watanzania wamekosa ubunifu na ni wachoyo wa kutumia maarifa waliyonayo katika
kujiendeleza na kuwaendeleza wengine.
Amina Issa, mkazi wa Tumbaku-Morogoro
alisema: “Nilitamani kuwa mjasiriamali wa aina nyingine mara baada ya biashara
ya kuendesha pikipiki kunishinda, niliwafuata watu wengi ili wanieleze manufaa
yanayopatikana katika biashara hii ya M-Pesa.
“Wengi hawakuniambia ukweli lakini
sikukata tamaa baaada ya kujua ukweli na kupata mafanikio ninajisikia furaha
sana kwani sasa maisha yangu yanaenda bila wasiwasi.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Vodacom, Joseline Kamuhanda, alisema wataendelea kuthamini na kutambua
mchango wa mawakala wao wote nchini kwa kuboresha maisha yao.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment