Mvujishaji wa siri za Marekani Edward
Snowden ukimbizini mjini Moscow
Wabunge
wenye ushawishi mkubwa katika bunge la Marekani wametupilia mbali ombi la
aliyekuwa mfanyakazi wa shirika la taifa la usalama la Marekani, NSA, Edward
Snowden kutaka msamaha.
Wabunge hao walieleza msimamo wao
kuhusu Edward Snowden katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS jana
Jumapili. Mwenyekiti wa kamati inayohusika na ujasusi katika seneti ya Marekani
Dianne Feinstein alisema kuwa badala ya kuvujisha siri kwenye vyombo vya
habari, Snowden angetoa malalamiko yake kwa siri kwenye kamati anayoiongoza.
''Alikuwa na nafasi, kama alitaka
kufichua maovu, kuipigia simu kamati ya ujasusi ya baraza la wawakilishi na ya
seneti, na kusema kwamba anazo taarifa ambazo angependa tuzifahamu. Hakika
tungekutana naye, kwa pamoja, au kila kamati kwa wakati wake. Lakini hakufanya
hivyo, na sasa baada ya kusabaisha matatizo makubwa kwa nchi yake, anataka
msamaha. Jibu langu ni hapana.'' Alisema Feinstein.
Naye mwenyekiti wa kamati ya ujasusi
katika baraza la wawakilishi Mike Rogers, amesema kumpa msamaha Edward Snowden
ni kitu kisichowezekana.
Alisema, ''Kama anataka kurudi
nyumbani, na kuwajibika kwa makosa yake ya kuiba taarifa za siri na kukiuka
kiapo chake, nitafurahi kuzungumza naye. Lakini anapaswa kuwajibika kwa yale
matendo yake na kama anataka kutoa sababu ya kuchukua hatua hiyo, hii ndio njia
sahihi ya kufanya hivyo.
Njia sahihi ya kulalamika
Mike Rogers aliongeza kuwa iwapo
Snowden anaamini kuwa yapo mapungufu katika mfumo wa ujasusi wa Marekani ambayo
alihitaji kuyaweka wazi, haikuwa busara kufanya hivyo kwa njia ambayo inaweza
kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani walio katika operesheni mahali kama
Afghanistan.
Majibu hayo ya wabunge wa Marekani
yametolewa siku chache baada ya mkutano kati ya Snowden na mbunge wa chama cha
watetezi wa mazingira cha Ujerumani, Hans-Christian Ströbele mjini Moscow.
Baada ya mazungumzo hayo, Snowden alimpa Stroebele barua ambamo alieleza kuwa
tayari kutoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani, kuweka wazi kile alichokiita
''uhalifu ambao huenda ni mkubwa''.
Tangazo la ukweli
Katika barua hiyo ya ukurasa mmoja,
Edward Snowden anaomba msamaha kwa mashitaka dhidi yake, kwa shutuma kuwa
alivujisha taarifa nyeti za Shirika la NSA kwa vyombo vya habari.
Mbunge Stroebele alikutana na Snowden
Alhamis iliyopita, kuzungumza naye kuhusu taarifa zilizochapishwa na vyombo vya
habari, kwamba NSA iliidukua simu ya mkononi ya kansela wa Ujerumani Angela
Merkel. Snowden aliahidi kutoa maelezo mbele ya bunge la Ujerumani, ikiwa
usalama wake utahakikishwa.
Taarifa zilizovujishwa na mfanyakazi
huyo wa zamani wa NSA, zimesababishwa miito ya nchi washirika kuacha kudukuana,
na zimeanzisha mchakato katika bunge la Marekani kutaka mfumo wa ujasusi wa
nchi hiyo ufanyiwe marekebisho.
Katika kile kilichoitwa ''tangazo la
ukweli'', ambalo lilichapishwa na gazeti la Der Spiegel la Ujerumani, Edward
Snowden alisema udukuzi wa mawasiliano ya halaiki ya watu unaweka kitisho kwa
uhuru wa watu kujieleza katika jamii ya kidemokrasia.
Mwandishi: Daniel Gakuba/DW English
website/rtre/afpe/ap
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment