na Betty Kangonga
MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu
za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe, amewataka Spika wa Bunge, Anne Makinda, na
naibu wake, Job Ndugai, kuacha kutumiwa na serikali kuingilia kamati za Bunge
wakati zikitimiza majukumu yake.
Akizungumza jana wakati wa ufunguzi
wa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za PAC na ile ya serikali za mitaa (LAAC),
Filikunjombe alisema mara nyingi kama kamati wamekuwa wakipokea simu kutoka kwa
viongozi hao zinazolalamikia utendaji wao.
Filikunjombe alisema kuwa hatua ya
kuruhusu vyombo vya habari kuingia wakati wa kuhoji mashirika na taasisi
mbalimbali za umma imesababisha tatizo hadi kufikia viongozi hao kuwapigia simu
na kuwataka kutofanya hivyo.
Alisema kuwa hatua hiyo inasababisha
kukosa uwajibikaji na uwazi katika masuala ya fedha za umma.
“Tunawaita watendaji waje kujieleza
mbele ya kamati juu ya matumizi ya fedha lakini cha kushangaza utaona unapigiwa
simu mara na Spika au naibu wake; sasa hii inaondoa dhana nzima ya
uwajibikaji,” alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Ludewa
(CCM), taasisi hizo zinapoomba fedha zinafanya hivyo mbele ya umma sasa
inashangaza kuhofu kuhojiwa wakati vyombo vya habari vikiwepo.
Alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi
hao kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini ili kuwa na
uwajibikaji.
“Tunaomba pia kuepuka kuzivunja
kamati hizi mbili, ni vyema zikaachwa ili zidumu kwa kipindi chote kuliko
kuzivunja kwa kuwa zina umuhimu zaidi katika usimamizi wa fedha za umma,”
alisema.
Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema kuwa ni muhimu Makinda akaona
umuhimu wa kuleta kamati nyingine ili kuwezesha shughuli zilizokuwa zikifanywa
na kamati ya POAC zikaweza kuendelezwa.
“Tunafahamu umuhimu wa kamati hiyo,
leo tunaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati zilizovunjwa, hivyo
Bunge linapaswa kuzingatia uamuzi unaofanywa,” alisema.
Utouh aliongeza kuwa ni vyema Bunge
likaona umuhimu wa kamati hizo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha ili zifanye kazi
zao kwa umakini.
Naye Mwenyekiti wa LAAC, Rajab
Mbarouk Mohamed, alisema kuwa kamati hiyo inasikitishwa na kitendo
kinachofanywa na ofisi ya Bunge kwa miaka miwili kushindwa kuwapa fedha ili
kuweza kukagua miradi ya maendeleo.
Alisema kuwa hivi sasa kamati
zimechoka kuwa washauri tu badala yake zimetaka kupewa meno ili ziweze kutembea
na askari polisi pindi zinapokwenda kufanya ukaguzi mbalimbali.
“Ili nidhamu irudi katika halmashauri
zetu tuna haja ya kupewa meno na kukabidhiwa polisi ili tunapokamata watendaji
wabadhirifu tuweze kuwakabidhi kwa vyombo vya dola na wakawekwa ndani ili
waogope,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Ndugai alikiri
kuwa huko nyuma sheria za Bunge zilikuwa haziruhusu vyombo vya habari kuingia
wakati idara mbalimbali zinahojiwa kuhusu matumizi.
Ndugai alisema kuwa kuanzia sasa
wanajaribu kuangalia namna ya kuweka uwazi katika suala hilo ili kuviruhusu
vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi ya fedha za umma.
“Juu ya suala la Utouh, nimelipokea;
ninaahidi kulifikisha Bungeni na tutatoa majibu muda si mrefu,” alisema.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment