na Danson Kaijage, Dodoma
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika
(CHADEMA), amesema migogoro iliyojitokeza wakati wa Operesheni Tokomeza
Majangili haiwezi kutenganishwa na agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya
Kikwete.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana
alipokuwa akifungua mafunzo ya wajumbe na viongozi wa CHADEMA kutoka kata 35
kati ya 37 zinazounda Jimbo la Dodoma.
Alisema pamoja na baadhi ya wabunge
wa CCM kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Khamis Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kuwajibika,
Rais Kikwete hawezi kuachwa kando.
Alisisitiza kuwa Rais Kikwete
asiwekwe kando kwani sababu kubwa ya mifugo ya wafugaji na wao wenyewe kuuawa,
kumetokana na udhaifu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayoongozwa na
Rais Kikwete.
Mnyika alimtaka Rais Kikwete
kutonyamaza bali atoe tamko kwanini Operesheni Tokomeza Ujangili imegeuka kuwa
tokomeza mifugo na mauaji ya wafugaji.
“Pamoja na ukweli kuwa baadhi ya
mawaziri wana udhahifu katika kusimamia operesheni hiyo, lakini Rais Kikwete
naye anapaswa kujiuliza na kuwajibika kwanini yametokea hayo na yeye amekaa
kimya hadi Bunge limefikia hatua ya kujadili jambo hili kwa uzito mkubwa?
“Haiwezekani Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa CCM na kiongozi wa nchi akanyamaza bila kutoa tamko, kwanini
matukio hayo yametokea badala ya kupambana na majangili askari wanapambana na
wafugaji na mifugo yao,” alisema.
Akiendelea kuzungumza na viongozi hao
wa kata, Mnyika alisema CCM pamoja na serikali yake haina nia njema na wafugaji
kwani kila kinachotendeka kina baraka ya serikali ya Rais Kikwete.
Aidha, alisema kuna kila sababu ya
viongozi wa CHADEMA kuhakikisha wanasimamia vema mchakato wa rasimu ya Katiba
mpya kwa kuhakikisha wanapiga kelele ili Katiba mpya iwe na kipengele cha
kumruhusu Mtanzania kumiliki rasilimali ardhi.
Alisema haiwezekani Mtanzania asiwe
na uhakika wa kumiliki ardhi, kwani kwa Katiba ya sasa ambayo ni mbovu inampa
madaraka makubwa na ardhi yote ni mali ya rais.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment