Waandishi habari wawili waliouwawa
nchini Mali
Watu wenye silaha wamewateka nyara na kuwauwa waandishi
habari wawili wa redio moja ya nchini Ufaransa ambao walikuwa wakielekea
kaskazini mwa Mali kwa shughuli za kikazi siku ya Jumamosi(02.11.2013).
Maafisa wa Ufaransa na wa Mali
wamesema kuwa watu hao wenye silaha waliwakamata waandishi hao wakati
walipokuwa wakitoka katika nyumba ya kiongozi wa waasi.
Vifo hivyo vinakuja siku nne baada ya
Ufaransa kusherehekea kuachiliwa huru kwa raia wake wanne ambao wamekuwa
wakishikiliwa kwa muda wa miaka mitatu na makundi ya washirika wa al-Qaeda
katika eneo la Afrika kaskazini.
Haikufahamika mara moja ni kundi gani
limewauwa waandishi habari hao wa radio ya kimataifa ya Ufaransa, Radio France
International. Ufaransa ilifanya operesheni ya kijeshi ya kuingilia kati
Januari mwaka huu katika koloni lake hilo la zamani kujaribu kuwaondoa
wapiganaji wa Kiislamu kutoka madarakani katika mji wa Kidal pamoja na miji
mingine katika eneo la kaskazini mwa Mali. Makundi yanayotaka kujitenga sasa
yamerejea katika eneo hilo.
Rais asikitishwa
Rais wa Ufaransa Francois Hollande
ameeleza masikitiko yake kutoka na tukio hilo la kuchukiza. Claude Verlon na
Ghislaine Dupont walikamatwa na watu kadha wenye silaha baada ya kumaliza
mahojiano , amesema afisa mmoja. Miili yao ilitupwa baadaye kilometa kadha nje
ya mji katika barabra inayoelekea Tinessako , katika eneo la mashariki ya mji
wa Kidal, kwa mujibu wa mtu ambaye aliona miili hiyo na maafisa wanne ambao
walielezwa kuhusu suala hilo.
Shirika la utangazaji la RFI
limemueleza Dupont mwenye umri wa miaka 51, na Verlon mwenye umri wa miaka 58,
kuwa wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu wakiwa na uzoefu wa miaka mingi
katika maeneo yenye changamoto. Dupont alikuwa mwandishi habari ambaye
"alikuwa anaipenda kazi yake pamoja na bara la Afrika ambapo alikuwa
akiandika habari zake tangu alipojiunga na RFI mwaka 1986," shirika hilo
limesema katika taarifa . Verlon alikuwa "ameyazowea mazingira magumu
duniani kote."
Masikitiko
Wafanyakazi wa shirika hilo,
"wameshtushwa mno , wamesikitishwa mno, wamechukizwa na kukasirika,"
taarifa hiyo imesema. Ufaransa ilianzisha uchunguzi wa kisheria kuhusiana na
utekaji nyara na vifo "vinavyohusishwa na makundi ya kigaidi,"
imesema ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali. Tuhuma katika mauaji hayo
ya Jumamosi haraka zimewaangukia wapiganaji wa Kiislamu.
"Kwa taarifa ambazo ninazo ,
shingo zao zimekatwa. Hatufahamu kwa hakika nani waliowakamata, lakini ripoti
tunazozisikia zinaonesha kuwa walikuwa ni makundi ya Waislamu wenye itikadi
kali," amesema Lassana Camara , naibu mkuu wa wilaya ya Tinessako.
Maafisa kadha wa Kidal waliohojiwa
kwa simu wamesema kuwa waandishi hao wa RFI walikamatwa baada ya mahojiano nyumbani
kwa Ambeiry Ag Rhissa, kaimu mkuu wa kundi la harakati za ukombozi wa Azawad,
ama NMLA, kundi la Watuareg linalotaka kujitenga ambapo waasi wake walilivamia
eneo la kaskazini mwa Mali mwaka jana.
Waasi hao baadaye walifukuzwa kutoka
katika eneo hilo la wapiganaji wenye mafungamano na al-Qaeda lakini sasa
wamerejea na kulidhibiti eneo la Kidal katika miezi ya hivi karibuni.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri : Bruce Amani
Chanzo: DWSwahili
No comments:
Post a Comment