Benki Kuu ya Tanzania.PICHA|MAKTABA
Na Florence
Majani, Mwananchi
Kwa ufupi
Ripoti hiyo ya Uhalifu wa Kiuchumi ya mwaka 2013 iliyotolewa
na Kampuni ya Uchunguzi wa Huduma ya Delloite imebaini kuwa watendaji wa ngazi
za juu wanahusika zaidi na uhalifu huo ukilinganisha na watendaji wa ngazi za
chini.
Dar es Salaam.Taasisi za Fedha nchini zimepoteza
kiasi cha Sh34.4 bilioni kuanzia kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi Oktoba
mwaka huu kutokana na wizi wa fedha katika taasisi hizo,ripoti mpya
imebainisha.
Utafiti huo uliofanyika katika nchi
za Kenya,Tanzania na Uganda umebainisha kuwa,Taasisi za Fedha za Afrika
Mashariki zimepoteza zaidi ya Sh471 bilioni sawa na (USD 30 milioni) kwa mwaka.
Hata hivyo benki hizo ziliweka wazi
upotevu wa Sh126.9 bilioni tu ambao ni robo ya upotevu huo wa zaidi ya Sh471
bilioni kwa kile kinachodaiwa kuhofia kupoteza wateja.
“Taasisi za fedha zinapoteza fedha
nyingi kutokana na teknolojia na watendaji wa ngazi za juu kuhusika kwa kiwango
kikubwa lakini hazitaki kukiri kwa sababu ya kuhofia kukosa wateja,” alisema
Robert Nyamu, Mkurugenzi wa Delloite, Afrika Mashariki.
Msemaji wa Benki Kuu ya Tanzania,Loy
Nabeta hakuwa tayari kuzungumzia upotevu huo na kusema kuwa ni suala
linalohitaji majadiliano ya kina na utendaji wa ngazi za juu.
Wimbi la wizi wa fedha katika benki
lilianza kupata umaarufu mwaka 2010 na Oktoba 2012 hadi Februari 2013,
inakadiriwa kuwa jumla ya Sh700 milioni zimeibwa katika benki mbalimbali kwa
nyakati tofauti.
Ripoti hiyo ya Uhalifu wa Kiuchumi ya
mwaka 2013 iliyotolewa na Kampuni ya Uchunguzi wa Huduma ya Delloite imebaini
kuwa watendaji wa ngazi za juu wanahusika zaidi na uhalifu huo ukilinganisha na
watendaji wa ngazi za chini.
“Wanapofanya uhalifu hujua namna ya
kuuficha na kuujadili na wasimamizi wa ndani bila kubainika.Wanajua mbinu na
mifumo yote ya kifedha na wanatumia fursa hiyo kuiba,” alisema Nyamu.
Watendaji waliotajwa kuhusika zaidi
na wizi huo wa fedha ni wale wa ngazi za juu wakiwamo wakurugenzi watendaji,
ofisa operesheni, wakurugenzi wa fedha, vitengo vya teknolojia na wakuu wa
vitengo wanatumia nafasi zao kufanya uhalifu wa fedha ukilinganisha na
wafanyakazi wa kati na ngazi za chini.
Wizi unaofanyika zaidi katika nchi za
Afrika Mashariki unatajwa kuwa ni wa fedha halali ambao ni zaidi ya asilimia 70
ya uhalifu wa aina zote wa kifedha.
Hata hivyo Nyamu alisema watendaji wa
ngazi za chini wanaweza kufanya uhalifu wa kiasi kikubwa cha fedha iwapo
wanajua namna ya kufanya hivyo.
Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa
Chuo cha usimamizi wa Fedha(IFM), Dk Eliamani Sedoyeka alisema ni kweli kuwa
watu wa ngazi za juu wanatumia nafasi zao kufanya uhalifu wa kifedha kwa sababu
wanaelewa kwa undani mfumo unavyofanya kazi na kutolea mfano i wizi wa Benki ya
Stanbic .
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment