Tuesday, November 5, 2013

SIMBA WATAFUTA AHUENI KWA ASHANTI




Wakati Simba ikitarajiwa kushuka uwanjani kesho kucheza na Ashanti United, Kocha Mkuu wa timu hiyo Abdalla King Kibaden amesema wanahitaji ushindi katika mechi hiyo hata kama hawatakaa kileleni.
Simba itashuka uwanjani kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kucheza na Ashanti United mechi ya mwisho ya kufunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Katika msimamo wa ligi hiyo Simba wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 21, huku Azam FC wakiwa vinara wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 26 sawa na Mbeya City tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wao wanashika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 25.

Kibaden alisema mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kwani wapinzani wao Ashanti sasa hivi wameamka na kucheza kandanda safi.
"Ni mechi ambayo tunatakiwa kushinda hata kama hatutakaa kileleni, isitoshe ni mechi ya mwisho ya kufunga mzunguko wa kwanza Mechi itakuwa na upinzani mkali sana," alisema Kibaden.

Alisema wanaendelea na mazoezi kama kawaida lengo likiwa ni kufanya vizuri katika mchezo huo, ambapo wachezaji wake wanaendelea vizuri kwa ajili ya mchezo huo licha ya mechi iliyopita kutoa sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar.
Mbali ya mechi hiyo mechi nyingine zitakazochezwa kesho ni kati ya JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Kagera Sugar na Mgambo Shooting Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na Ruvu Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Siku inayofuata Azam itacheza na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora
Chanzo: Majira

No comments: