Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akichangia hoja kwenye
mjadala wa kupitisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2014/15, mjini
Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Waandishi
Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam/Dodoma.Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa amesema ana shaka kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now),
utafanikiwa kutokana na Kitengo cha Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya
Miradi ya Maendeleo kilicho chini ya Ofisi ya Rais (PDB) kukosa meno.
Akichangia mjadala wa hoja ya
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015, Lowassa alisema
tatizo kubwa linaloikabili nchi ni viongozi kushindwa kutekeleza mipango
mbalimbali ya maendeleo.
“Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo
mengi lakini hakuna utekelezaji,” alisema Lowassa wakati akichangia mjadala huo
uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen
Wassira, wiki iliyopita.
Mbunge huyo wa Monduli (CCM), Lowassa
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Mambo ya Nje alisema itakuwa vigumu
kwa PDB kutekeleza wajibu wake wakati hakina meno ya kusimamia utekelezaji wa
mipango ya Serikali.
Kitengo cha PDB kinachoongozwa na
Omar Issa kiliundwa mwaka huu na kutengewa kiasi cha Sh29 bilioni na
kulalamikiwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika wakati wa kikao cha
Bunge cha Bajeti 2013/14.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni
sehemu ya jitihada za Serikali kuinua uchumi kutoka wa chini hadi kufikia wa
kati ifikapo mwaka 2025.
“Nataka mjiulize maswali machache.
Je, hawa PDB wana meno?” alisema Lowassa na kuongeza:
“Tunazungumza lakini mjue kuwa
`discipline’ (nidhamu) ya wenzetu wa Malaysia ni tofauti na hapa kwetu. Hapa
kuna uswahili mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, mnaamua bila kutekeleza.”
Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Lowassa aliitaka Serikali kuwa na
mipango michache ambayo itakayoweza kuifuatilia kwa ukaribu na kuitekeleza.
Alipendekeza kuwa ajira, elimu na kuendeleza reli kuwa vipaumbele muhimu.
“Kinatakiwa chombo ambacho kinaweza
kufanya uamuzi mgumu unaotekelezeka kwelikweli. Bila kuwavika joho la kufanya
uamuzi ili kuwarahisishia utekelezaji wa kazi yao na wakawa na ‘function’
itakuwa ni kazi bure. Ni uamuzi mzuri kuanzisha mpango huu lakini msipoangalia
itakuwa kazi bure. Lazima wawe na meno ya kuuma mkishakubaliana mambo
yafanyike.”
Kila mtu analalamika
Lowassa alisema sasa Tanzania imekuwa
nchi ya kila mtu kulalamika, kuanzia viongozi hadi wananchi.
“Wananchi na viongozi wote
wanalalamika haiwezekani kukawa na jamii ya aina hii, lazima awepo mtu mmoja
anayefanya uamuzi na anayechukua hatua. Bila kuchukua hatua tutaendelea
kulalamikiana tu” alisema.
Mpango wa Matokeo Makubwa uliingizwa nchini kwa kurudufiwa
kutoka Malaysia, ambayo ilipopata uhuru mwaka 1957 ilikuwa katika kiwango sawa
na Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi lakini sasa ina rekodi ya juu kiuchumi
barani Asia. Mpango huu pia unatekelezwa Nigeria na Rwanda na umeonyesha
mafanikio makubwa katika nchi hizo.
Katika kutekeleza mpango huo, Serikali imeanza na wizara
sita; Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kilimo, Chakula na Ushirika, Maji, Uchukuzi,
Fedha na Nishati na Madini.
Ajira
Akizungumzia suala la elimu, Lowassa alisema: “Huwezi
kuzungumza mipango bila kuzungumza ajira, kuna Watanzania wengi waliomaliza darasa
la saba, kidato cha nne na sita wapo mitaani na hawana ajira. Tusipoangalia
watakuja kula sahani moja na sisi.”
Alisema katika mkutano wa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la
Fedha Duniani (IMF) mwaka huu, walizungumzia mdororo wa uchumi kwa nchi za Ulaya
na moja ya nchi hizo ambayo ni Hispania, ilieleza jinsi ilivyoweza kujinasua
kwa kuweka kipaumbele cha ajira.
“Hispania walitoa mfano kuwa walikuwa na ukosefu wa ajira
kwa asilimia 50, waliamua katika bajeti yao kujikita katika kuzalisha ajira.
Kila mwekezaji aliyekwenda katika nchi hiyo alipewa masharti ya kuwekeza katika
ajira ya vijana. Kimsingi tunatakiwa kuwa na takwimu za kujua tumezalisha ajira
ngapi ndipo tutajua uchumi wetu unakua kwa kiasi gani,” alisema.
Lowassa alisema baada ya miaka mitatu nchi hiyo imetoka kuwa
miongoni mwa nchi zisizo na ajira na kusisitiza kuwa mipango mingine ni migumu
kutekelezeka kama nchi haitakuwa na ajira.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa na Mkuu wa
Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kutokana na kitendo chao cha kuwapa ajira
wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu baada ya kuwapatia matrekta na mashamba.
Elimu
Lowassa alisema kuna tatizo la msingi katika elimu ya
Tanzania. “Nilitegemea wahusika wangepata taarifa ya Tume ya Serikali
kuchunguza kushuka kwa kiwango cha elimu ili kujua matatizo yaliyopo katika
elimu na nini cha kufanya.”
Mwanzoni mwa mwaka huu Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda aliunda tume ya watu 15 kuchunguza sababu za idadi kubwa ya
wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika matokeo ya mtihani huo mwaka 2012.
Tume hiyo tayari imeshakamilisha kazi
na kukabidhi ripoti hiyo serikalini, lakini mpaka sasa bado haijawekwa
hadharani.
“Haitoshi kumchukua mwanafunzi
aliyemaliza chuo kikuu wakati akienda katika soko la ajira wakati shahada yake
hamsaidii, mtu ana shahada lakini kazi hakuna.”
“... Kunatakiwa kufanyika mjadala
nchi nzima kuzungumza juu ya matatizo na nini kifanyike. Nchi isipokuwa makini
katika hili itaachwa katika ushindani uliopo sasa kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC).”
Awafagilia Magufuli, Mwakyembe
Akizungumzia uendelezaji wa Reli ya
Kati alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli kujenga barabara, alisema zinaharibika kwa kasi kutokana na kuzidi kwa
kiwango cha uzito wa malori.
“Reli ya Kati inatakiwa kuangaliwa
kwa haraka maana malori yanayotembea katika barabara yatapungua kwa kuwa mizigo
itakuwa inachukuliwa na treni,” alisema. Licha ya kusifu kazi inayofanywa na
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe Lowassa alisema foleni jijini Dar es
Salaam zinashusha uzalishaji, kwani watu wengi wanatumia muda mwingi barabarani
kuliko kufanya shughuli za maendeleo.
“Serikali haiwezi kukaa hivi hivi,
‘this is a disaster’ (hili ni janga), mtafute njia ya kuangalia mnafanyaje
kumaliza foleni ya Dar es Salaam, jambo hili lifanyike sasa,” alisema.
Uamuzi mgumu
Lowassa alisema pia Tanzania
haitakiwi kuendelea kulumbana na Uganda, Rwanda na Kenya zinazotaka kuitenga
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), badala yake ichukue uamuzi mgumu wa
kushirikiana na nchi nyingine.
“Wao wameamua kuanzisha ushirikiano
na Sudan Kusini, Tanzania inaweza kuanzisha ushirikiano na Jamhuri ya
Kidemokrasia Kongo (DRC) ambako ni kuzuri zaidi na kikubwa kinachotakiwa
kufanyika ni kuifufua Reli ya Kati,” alisema.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment