Raia watatu wa China wamekamatwa
nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa
katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
Pia watuhumiwa hao wa Kichina
wamekutwa na fedha taslim shilingi milioni 30.2 za Kitanzania, sawa na zaidi ya
dola elfu 18 za Kimarekani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki akifuatana na kikosi maalum cha polisi, waliwanasa Wachina hao
katika makaazi yao jijini Dar es Salaam.
Waliokamatwa na meno hayo ya tembo
wametajwa kuwa ni Chen Jinzha, Huang Qin na Xu Fujie wote kutoka mji wa
Guangdung nchini China.
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi
katika nyumba walimokamata meno ya tembo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya
kuingiza vitunguu swaumu nchini Tanzania kutoka China huku wakisafirisha nje
makombe ya konokono wa baharini.
Akizungumza na waziri Kagasheki,
mtuhumiwa Huang Qin amesema shehena yote iliyokamatwa ndani mwake ilikuwa
ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Kukamatwa kwa meno haya ya tembo
Jumamosi, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha "Operesheni
Tokomeza Ujangili", ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini
kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama
wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa kwa meno ya
tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20,
2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani
yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata
raia mmoja wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi
milioni 18 sawa na dola za Kimarekani zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda
nje.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment