Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya
CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: "Kwanza ni kweli kwamba kuna
ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama,
wanataaluma, baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja
wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa."
Aliongeza: "Mwanzoni sikuona
uzito sana, yaani sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni
kwamba ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa
ninalitafakari kwa kina".
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais,
atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na chama hicho,
lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa akijibu hoja za gazeti
hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba ameanza
harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua
yake hiyo imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari
wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini, wakiwamo wale
wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa
katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa
masuala ya kisisa wanasema 'katika siku za karibuni mwenendo wake unaashiria
kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye mipango
yake binafsi ya kisiasa".
Habari ambazo Mwananchi imezipata
zinasema mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan
wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani wakimlalamikia
kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo
yake anasema hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote
kwani yeye haamini katika makundi. "Ninaamini katika kundi moja, nalo ni
CCM," alisema.
Aliongeza: "Kwa hiyo mtu yoyote
akinikasirikia kwa sababu zozote zile za kisiasa nitamshangaa maana sijawahi
mahali popote na kwa namna yoyote kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi
fulani, au kundi la mtu yeyote."
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka
za mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu wa
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na mambo
mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa wajumbe wa mkutano
huo.
Imethibitika kwamba mpango huo
ulikuwa ni wake binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako
naye katika harakati za kumuunga mkono Lowassa.
Tukio jingine ni lile la vijana
waliojitambulisha kuwa viongozi wa vyuo vikuu nchini kutangaza katika mkutano
wao mjini Morogoro kwamba watamwomba Makamba awanie urais katika Uchaguzi Mkuu
ujao, kutokana na kile walichodai kwamba ni matokeo ya kura walizopiga baina ya
kiongozi huyo na viongozi wengine vijana; John Mnyika na Zitto Kabwe wa
Chadema.
Wapinzani wake wanaamini kwamba tamko
la vijana hao zilikuwa mbinu binafsi za Makamba kutaka kuonyesha kwamba naye
anakubalika na pengine maandalizi ya kujiengua rasmi kutoka katika kambi yake
ya awali.
Wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu
ya miaka 14 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makamba alikuwa Butiama
mkoani Mara ambako mbali na kushiriki Ibada ya kumwombea Baba wa Taifa, pia
alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la kumuenzi kiongozi huyo.
Kuhusu baadhi ya makada wenzake
kukasirishwa na mwenendo wake kisiasa, Makamba alisema: "Hata mimi
nimesikia kama wewe unavyosema umesikia, inawezekana wanakasirishwa na mvumo
maana ndani ya chama chetu watu wanazungumza sana, tena hadharani kwa hiyo
katika mazingira hayo taarifa zinaweza kumfikia yeyote kama zilivyokufikia
wewe".
Alitetea hatua yake ya kugawa simu kwenye
mkutano wa UVCCM akisema alikuwa akitimiza ahadi aliyoitoa wakati wa semina ya
vijana hao Februari mwaka huu mjini Dodoma, pale walipomuomba kuwasaidia ili
waweze kutekeleza matakwa ya ushauri wake wa kukitetea CCM katika mitandao ya
kijamii.
"Mimi kwa nafasi yangu nikiwa
Naibu Waziri wa masuala ya teknolojia, nikiombwa kusaidia lolote katika eneo
langu ndani ya chama sioni tatizo ilimradi niwe na uwezo nalo, kwa hiyo
nilitimiza ahadi yangu tena kwa uwazi sikufanya kwa kificho,"alisisitiza.
Makamba ni mwanasiasa wa tatu kijana
kutajwa kuwa huenda akawania urais, wengine wakiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine ambao wameishaonyesha nia ya
kuutaka urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Lowassa.
Vita ya urais imekuwa ikikiumiza CCM,
ambapo Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania Bara), Philip Mangula aliwahi
kukaririwa akiwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza kupiga mbio za
kuusaka uongozi huo kuwa hawatavumiliwa, kwani harakati hizo zimekuwa kichocheo
cha mgawanyiko ndani ya chama.
Chanzo:
Mjengwablog
No comments:
Post a Comment