Mizengo Pinda Kushindwa kuzuia mauaji kwa wananchi wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili Kauli aliyoitoa bungeni kuwa
wahalifu wapigwe tu, inatumiwa vibaya na askari wanaoendesha Operesheni
Tokomeza Ujangili. Picha na Maktaba
Na Habel
Chidawali, Mwananchi
Dodoma. Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na
mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David wameingia matatani kutokana na shinikizo
linalowataka wang’oke katika nafasi zao.
Pinda pamoja na mawaziri hao
wanatakiwa kuachia ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo
na baadhi ya watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na
wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa
upande mwingine.
Jana wabunge walicharuka na kuwataka
mawaziri waliohusika katika Operesheni Tokomeza Ujangili wawajibishwe wakieleza
kutoridhishwa na maelezo waliyoyatoa mapema jana, baada ya kipindi cha maswali
na majibu.
Kelele za wabunge zilizuka baada ya
wabunge kuanza kuchangia maelezo ya Serikali kuhusu migogoro ya wafugaji na
wakulima, hifadhi za wawekezaji na maelezo ya Serikali kuhusu Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala
huo ni Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake
alitoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile ambacho
alikiita kuwa ni unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake
kwa Serikali kuwa ilifanya operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi
hivyo kuwaathiri wananchi wasiokuwa na hatia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya
kuahirisha kikao cha Bunge jana mchana aliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya
Bunge kwa ajili ya kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakati
‘madudu’ ya Operesheni Tokomeza Majangili yatachunguzwa kupitia Kamati ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Chimbuko la hoja
Jana asubuhi kabla ya Bunge kuanza
kikao chake, Spika Makinda alitoa taarifa kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi
kingekutana wakati kipindi cha maswali na majibu kikiendelea, kwa lengo la
kutoa mwelekeo wa mjadala wa hoja za dharura.
Hoja hizo ni zile zilizotolewa na
wabunge wawili kwa nyakati tofauti; Alphaxard Kangi Lugora wa Mwibara (CCM)
kuhusu Operesheni Tokomeza Majangili na Saidi Nkumba wa Sikonge (CCM), kuhusu
vita baina ya wakulima na wafugaji.
Kamati hiyo ilikutana baada ya
kipindi cha maswali na majibu na Spika Makinda alitoa taarifa za kusitisha
shughuli nyingine, ili wabunge waweze kujadili masuala hayo ambako kabla ya
kuanza mjadala aliwaita mawaziri kutoa taarifa zao.
Alianza Waziri wa Maliasili na
Utalii, Balozi Kagasheki ambaye katika maelezo yake alihitimisha kwa kutangaza
kusitisha Operesheni Tokomeza ili kupitia mpango huo na kufanya maboresho ili
kuondoa upungufu uliopo.
Licha ya kueleza sababu nyingi
zilizofanya Serikali kuendesha operesheni hiyo, alisema ina manufaa makubwa
katika kuokoa wanyama aina ya tembo, lakini waziri alihitimisha kwa kusema
itakuwa ni busara kuifanyia tathmini wakati ikiendelea, hivyo kutangaza
kuisitisha mara moja.
Kwa upande wake Dk Mathayo alitoa
maneno ya kuomba radhi na kuwapa pole watu waliopatwa na usumbufu ikiwa ni
pamoja na kupoteza mali zao na mifugo.
Mathayo aliwaeleza wabunge kuwa
Serikali imepanga kujenga malambo katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya
kuwasaidia wafugaji kupata maji ili kupunguza safari za kuhamahama kutoka eneo
moja kwenda jingine.
Shinikizo kwa Pinda
Baada ya kumaliza hotuba zao, wabunge
kadhaa walipata nafasi ya kuchangia maelezo hayo huku wengi wakielekeza shutuma
zao kwa mawaziri hao na wenzao wa Mambo ya Ndani ya Nchi na yule wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa.
Wabunge wawili wa Chadema, Paulina Gekul
(Viti Maalumu) na John Shibuda (Maswa Mashariki) walitaka Waziri Mkuu Pinda
ajiuzulu kutokana kushindwa kwake kudhibiti mauaji na mateso kwa wananchi.
Gekul alisema kinachotokea sasa ni
utekelezaji wa kauli ya Pinda aliyoitoa bungeni akisema wahalifu wapigwe tu
pamoja na ile ya Kagasheki aliyoitoa mjini Arusha akisema majangili
watakaokamatwa wamalizwe hukohuko kwenye hifadhi.
Mbunge huyo alieleza operesheni hiyo
kwamba imesababisha mauaji ya watu wasio na hatia ikiwemo mama Emiliana ambaye
alifuatwa akiuza nyanya, lakini akateswa hadi kufa na hadi sasa mwili wake bado
uko katika Hospitali ya Babati baada ya wananchi kugoma kuuzika.
Shibuda kwa upande wake alisema Pinda
anapaswa kufungua milango kwa mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu haraka, kutokana
na kulea uzembe ambao umesababisha madhara makubwa kwa wafugaji.
Shibuda alisema kuwa Wizara ya Mifugo
imekuwa na mtazamo hasi lakini akasisitiza kuwa uzembe wa viongozi wa ngazi za
mikoa, wilaya hadi vijiji unatokana na ukimya wa Pinda ambaye anashindwa
kuchukua hatua yoyote dhidi yao.
Wabunge wengine
Kwa upande wake Nkumba aliunga mkono
kuundwa kwa kamati teule, lakini akasisitiza kuwa mawaziri hao wanne wana hoja
za kujibu ndani ya chama tawala CCM na kwa Rais, vinginevyo Serikali haipaswi
kuendeshwa na viongozi wazembe wa aina hiyo.
“Mawaziri mnaosimamia jambo hilo
mnayo hoja ya kujibu kwa chama chenu tena bahati nzuri wote mnatoka CCM, ambao
ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, ninyi wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Maliasili na Utalii, nasema hatuko
pamoja na watu wazembe hata siku moja,” alisema Nkumba.
Mbunge huyo alionya kuwa umefika
wakati ambao Serikali inatakiwa iache tabia ya kuwadanganya wabunge kuwa
itapeleka taarifa bungeni, lakini mambo yakishapoa basi inakaa kimya na akataka
maelezo ya kina majangili wakubwa wako wapi, na kwa nini wasikamatwe na badala
yake kinachofanyika ni kuendelea kuwatesa wasiokuwa na hatia, kisha akashawishi
wabunge wote wazikatae taarifa za mawaziri hao.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola
alizikataa taarifa za mawaziri wote wawili kwa madai ya kupikwa na kujaa giliba
za kuwahadaa wananchi.
“Mawaziri hawa wataponea wapi katika
mkono huu, watu wamekufa, wameteswa, mifugo imeporwa na mingine kupigwa risasi
wao wapo tu, nasema wataponea wapi ikiwa ushahidi wote uko hapa,” alisema
Lugola na kuongeza:
“Mawaziri hawa wataponea wapi kama
damu ya Dasu Lutaligula (Kilombero), Madirisha Luchagula (Mulele), Baya Tambi
(Ulanga) wafugaji watano waliokufa huko (Mtimbira- Ulanga ), vilema vya kudumu
Luhende, Ofisa Tarafa (Mpimwe) Diwani wa Maji Moto, wafugaji watano wa Mtimbira
waliopata vilema kutokana na waliyotendewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi,
hivi wataponea wapi kwa damu za hao?”
Alisema zaidi ya ng’ombe 500 walipigwa
risasi katika mpango wa mradi wa watu wachache wa kutaka kujinufaisha wenyewe
ama kwa kushirikiana na viongozi wa juu.
Aliwatuhumu askari wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), polisi na askari wa wanyamapori, kuwa wamekuwa
wakiua watu ovyo na wengine kubakwa, lakini Serikali inawakingia kifua hali
inayoonyesha kuwa kuna udhaifu ndani ya Serikali.
Katika michango yao, Mbunge wa Viti
Maalumu, Ester Bulaya (CCM) alisema maelezo yaliyowasilishwa na mawaziri ni
mzaha, huku akiwaonya mawaziri kuacha tabia ya kupuuza hoja za wabunge, kwani
wanapozungumza huwa tayari wamefanya utafiti.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu,
Magdalena Sakaya (CUF) na Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia (NCCR-Mageuzi),
walisema yote yametokea kutokana na uzembe wa viongozi ikiwemo mawaziri
kushindwa kutimiza wajibu wao.
Hadidu za rejea
Jana jioni Spika wa Bunge, Anne
Makinda alimpa nafasi Profesa Msola, ili aelezee malengo ya kamati teule
itakayoundwa ambapo alisema itakuwa na jukumu la kuchunguza na kuchambua sera
mbalimbali zinazohusu ardhi, kilimo, mifugo, maji, wanyamapori na uwekezaji ili
kubaini kasoro za ardhi, hatimaye kuleta mapendekezo bungeni yatakayoondoa
migogoro ya ardhi inayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, hifadhi, uwekezaji
na watumiaji wengine wa ardhi.
Alizitaja hadidu za rejea za kamati
teule kuwa ni kuchambua sera mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi
kubainisha kasoro zilizopo katika sera hizo, kuchunguza mikakati iliyowekwa na
Serikali, kuchambua mikakati yote ya Serikali ya kusuluhisha migogoro ya wakulima
na wafugaji.
Nyingine ni kuchambua mikakati ya
kulinda vyanzo vya maji, uharibifu wa mazingira na kutoa mapendekezo
yatakayoondoa migogoro yote kudumisha uhusiano mzuri na utengamano na mambo
mengine ambayo kamati itaona yanafaa.
Akiboresha hadidu za rejea Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema ni vyema kamati teule hiyo ikapitia
ripoti mbalimbali tume na kamati zilizoundwa kuchunguza suala ya matumizi ya
ardhi ikiwemo ya Profesa Shivji.
Alisema kuwa kumekuwa na kawaida ya
kuunda tume ambazo zimekuwa ni siri na utekelezaji wake hakuna.
Mnyika alisema kuwa ni vyema katika
kuongeza hadidu za rejea ya kushughulikia uwajibikaji pale ambapo kuna kasoro
za utendaji.
Mbunge wa Tunduru Abdallah Mtutura
(CCM), alisema wapo watu ambao wameuawa kwa kisingizio kuwa ni majangili huku
wengine wakijificha maporini kuogopa operesheni hiyo.
Aliunga mkono kuongezwa kwa hadidu ya
kuchunguza mauaji na watu walioteswa katika operesheni hiyo.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama
(CCM), alitaka kuwepo kwa muda maalumu wa kamati teule kufanya kazi kwa kuwa
jambo hilo ni zito.
Alisema kumekuwa na tume nyingi
ambazo hazijaonyesha matokeo yake na kutaka kamati hiyo itakayoundwa iwe ya
mwisho katika utekelezaji.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses
Machali (NCCR- Mageuzi), alisema operesheni hiyo imefanya zaidi ya ugaidi na
unyama na kuomba waliohusika na mauaji na utesaji wa watu kupimwa akili.
Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni,
Habib Mohamed Mnyaa, (CUF), alitaka kuwepo kwa fidia kwa watu walioathirika na
operesheni hiyo.
Akihitimisha hoja hiyo, Profesa Msola
alisema mapendekezo yote yataingizwa katika hadidu za rejea ili yasaidie katika
utendaji wa kamati hiyo teule.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, alisema majina ya wabunge watakaounda kamati hiyo, yatatajwa Jumatatu
ijayo.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment