Spika wa Bunge Anna Makinda akiongoza shughuli za Bunge
Bungeni, mapema wiki iliyopita baadhi ya wabunge walikuja na hoja ya kutaka
kumng'oa Spika huyo bungeni. Picha na Maktaba
Na Neville
Meena, Mwananchi
Dodoma. Mchakato wa kumng’oa madarakani
Spika wa Bunge, Anne Makinda ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis
Kigwangalla (CCM), huenda usifanikiwe kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo
kupingwa na baadhi ya wabunge wenye ushawishi mkubwa katika Bunge.
Wabunge wameanza kumpinga hadharani
kuhusu suala hilo ambalo jana mjadala wake uliyateka makundi ya wabunge
waliokuwa wakihudhuria vikao vya kamati mbalimbali wakati wakiwa kwenye
mapumziko.
Katika viwanja vya Bunge jana, gazeti
hili liliwashuhudia Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na swahiba wake
kisiasa, Kangi Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) wakikataa kusaini
karatasi waliyopelekewa kuunga mkono kung’olewa kwa Spika.
Baadaye kwa nyakati tofauti walisema
“hoja hiyo haina mashiko” na kwamba hawakutumwa na wapigakura wao kuwania posho
bungeni.
Wabunge hao walikuwa wakirejea moja
ya hoja za Dk Kigwangalla kwamba Makinda amekiuka kanuni kwa kuidhinisha malipo
ya Sh430,000 kama posho kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na
wajumbe wa kamati nyingine ambao malipo yao ni Sh180,000 kwa siku.
Wengine wanaompinga Kigwangalla ni
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) na yule wa Kigoma Kusini, David
Kafulila (NCCR - Mageuzi), ambao pia walisema hawaoni sababu za msingi za
kumwondoa Makinda madarakani.
Rage kwa upande wake alisema haoni
sababu za msingi za kutaka kumwondoa madarakani Makinda, wakati Kafulila
alisema hilo ni suala la WanaCCM, kwani hata Spika aking’olewa atakayeziba
pengo hilo hawezi kutoka upinzani.
“Kama akitoka Makinda ataingia mtu wa
opposition (upinzani) yeyote basi ningeweza kusaini, lakini ninachojua ni kuwa
kama wakifanikiwa kumtoa watakaa kwenye Party Caucus (kikao cha chama) na
watateua mwingine kutoka miongoni mwao na mimi simwamini mbunge yeyote wa CCM,”
alisema Kafulila.
Filikunjombe na Lugola
Kwa upande wake Filikunjombe alisema
hoja ya Dk Kigwangalla imejengwa katika msingi hafifu na kwamba “haizingatii
masilahi mapana ya nchi, bali masilahi binafsi kwa mtazamo finyu wenye lengo la
kujitafutia umaarufu”.
“Bunge ni taasisi kubwa ambayo
haiwezi tu kuingia katika mtego wa kuenguana kwa sababu ya posho. Watu wa
Ludewa watanishangaa leo hii wakisikia kwamba eti nimesaini kumwondoa Spika
madarakani kwa sababu ya posho,” alisema Filikunjombe na kuongeza: “Kama hoja
ingekuwa ni kumtoa Spika kwa sababu anaipendelea na kuitetea Serikali bungeni
kana kwamba yeye ni waziri, basi hoja kama hiyo mimi ningeweza kuiunga mkono,
lakini siyo suala la posho”.
Kuhusu hoja kwamba Spika Makinda
alikiuka kanuni kwa kumteua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti badala ya kuchaguliwa kwa kura, Filikunjombe
alisema wanaopaswa kulalamika kwanza ni wajumbe wa kamati hiyo na siyo mtu
mwingine yeyote.
Kwa upande wake Lugola alisema msingi
wa hoja ya Dk Kigwangalla ni masilahi binafsi na kwamba ni mapambano ya kuwania
kupata kiwango kikubwa cha posho, suala ambalo kwa sasa siyo ajenda ya kitaifa.
“Kama kweli mtoa hoja angekuwa ana
nia ya dhati na uchungu wa nchi hii, angetuunga mkono katika hoja ya kutaka
kumwondoa Waziri Mkuu, lakini hakufanya hivyo sasa iweje leo anataka tumuunge
mkono katika masuala ya posho?” alihoji Lugola.
Wabunge hao walisema fedha
wanazipenda, lakini siyo kipaumbele katika kutekeleza yale waliyotumwa na
wanaowawakilisha bungeni. Hata hivyo Dk Kigwangalla aliwapuuza wabunge hao
akisema kuwa anayetaka asaini na asiyetaka asisaini na siyo kumshambulia na
kumbeza.
Vikwazo vingine
Mchakato wa kutaka kumg’oa Spika pia
unaweza hata usifike katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na
badala yake kuishia Ofisi ya Katibu wa Bunge ambako bado hoja yake inafanyiwa
kazi na wataalamu wa ofisi hiyo.
Hadi jana mchana Dk Kigwangalla
alikuwa bado hajapokea majibu kutoka ofisi ya katibu huyo na aliliambia gazeti
hili kuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alimwarifu kuwa “wataalamu
walikuwa bado wanaifanyia uchambuzi hoja yake hiyo”.
Dk Kashililah kwa upande wake
aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa: “Ni kweli hoja yake (Dk Kigwangalla)
tumeipokea na tunaifanyia kazi, tukimaliza tutamwarifu matokeo ya uchambuzi
wetu”.
Wakati Dk Kigwangalla ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akisubiri
majibu kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge, alisema tayari alikuwa amekusanya saini
za wabunge wapatao 110 ambao wanamuunga mkono katika harakati zake.
Miongoni mwa hoja za mbunge huyo ni
kwamba Spika amekuwa akivunja masharti ya Kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya
namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura kwa kuzuia mijadala hiyo.
Hata hivyo hatua ya Spika Makinda
kuruhusu mijadala kuhusu migogoro baina ya wakulima na wafugaji na ile
inayohusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili juzi, inaweza kutumika
kama kigezo cha kuiweka kando hoja ya Dk. Kigwangalla.
Habari ambazo gazeti hili limezipata
zinasema katika mazingira hayo, Ofisi ya Katibu wa Bunge inaweza kutumia sababu
hiyo pamoja na nyingine za kiufundi kuiweka kando hoja mbunge huyo, na kuzuia
isipelekwe katika kamati husika kama kanuni zinavyoelekeza.
Kikwazo kingine ni ukimya wa Kambi ya
Upinzani Bungeni ambayo hadi sasa imekaa kimya, ikiwa ni dalili ya kuwaacha CCM
“waumane” wao kwa wao.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment