na Happiness Mtweve
WIKI moja tangu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome, atangaze mfumo mpya wa
upangaji alama za matokeo ya wanafunzi wa sekondari kwa kufuta daraja sifuri na
kuanzisha daraja la tano, naibu waziri ameibuka na kupingana naye.
Naibu waziri huyo, Philipo Mulugo,
aliibua mkanganyiko huo bungeni jana, akisema si kweli kwamba serikali imefuta
daraja la sifuri katika mitihani ya kidato cha nne kama ilivyoeleweka.
Kutokana na kukinzana huko, Spika wa
Bunge, Anne Makinda aliiagiza serikali kuleta bungeni mabadiliko ya madaraja
hayo ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita yaliyotangazwa
hivi karibuni.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya
Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kuweza kupata majibu ambayo
yanaridhisha,” alisema.
Awali akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), Mulugo alisema taarifa
zilizoenea kwamba daraja la sifuri limefutwa si za kweli.
Katika swali lake, Magige alitaka
kujua kama uamuzi wa serikali wa kushusha madaraja katika mitihani ya kidato
cha nne lengo lake ni kuwaokoa wanafunzi wanaofeli.
“Serikali haijafuta divisheni sifuri
na wala hakuna daraja la tano, yaliyopo ni la kwanza, pili, tatu, nne na sifuri
kama kawaida,” alisema.
Alisema unamuzi wa kushusha madaraja
uliofanywa haukuwa na lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofeli bali ni kuondoa mrundikano
wa alama katika daraja moja.
Alisema serikali imeweka madaraja
mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi kutoka daraja moja kwenda jingine na
kwamba hata hivyo alama za ufaulu bado ni 40 ambazo ni daraja la C.
Awali akijibu swali la msingi la
Magige, Mulugo alisema serikali haina mpango wa kuanzisha programu maalumu hasa
za ufundi kwa wanafunzi waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
“Kwa mwaka 2013, jumla ya wanafunzi
60,507 wa kujitegemea, wamejisajili kufanya mtihani huo, watahiniwa 3,578
wakiwamo wasichana 2,020 na wavulana 1,558 waliofeli katika mtihani wa kidato
cha nne mwaka jana wamejisajili kurudia mtihani huo,” alisema.
Alisema kwa sasa katika vyuo vya
Ufundi Stadi kuna programu za fani mbalimbali za muda mfupi na muda mrefu ambazo
wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na sekondari wanaweza kujiunga kwa vile
mafunzo yatolewayo katika vyuo hivyo huzingatia stadi moja tu.
“Serikali imekuwa ikiongeza na
kuboresha vyuo vya ufundi na kuweka mazingira rahisi kwa wanafunzi ili waweze
kupata stadi mbalimbali,” alisema.
Mulugo aliongeza kuwa kati ya mwaka
2010 hadi 2012, serikali kupitia VETA imesajili jumla ya vyuo vya Ufundi Stadi
75 sawa na asilimia 75 na asilimia 10.8 ya vyuo 618 vilivyokuwapo.
Naibu waziri huyo alifafanua
kuwa katika kipindi hicho, jumla ya vyuo vinane sawa na asilimia 3.2 ya
vyuo 248 vilivyokuwepo vilisajiliwa na NACTE.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment