“Taarifa ya Chadema
inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu
tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” Zitto
Na Mwandishi
Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika sura mpya baada ya viongozi
wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu,
Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi wa chama hicho wakitaka uikane taarifa
inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa
kupokea fedha na kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari
`Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na
Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani
na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni
inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416
milioni) huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo
zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa
nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo
ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari jana, Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya
kweli au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba
chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka
2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya
kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha
na kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa
katika kipindi ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na
Uingereza ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika
nchi hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo
lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya
kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza Zitto
katika taarifa yake.
Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na
Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala
hilo.
“Hasa pale ambapo tumeambiwa waraka
huu umetoka makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti iliyosheheni
watu mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu katika idara hii
kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa yanayokigusa chama, vipi
makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?” aliandika Dk Mkumbo kwenye ukurasa wake
wa mtandao wa Facebook jana na kuthibitisha kwa simu.
Dk Kitila alisema pamoja na umaskini
wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
“Taarifa zinazosambazwa kuhusu mimi
ni za uongo wa kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni
wazi kwamba wanaosambaza habari chafu kunihusu hawanijui na ndiyo maana
wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi Kitila Mkumbo naweza kuhongwa Sh200,000.”
Alihoji pia Chadema ilikuwa na siri
gani za hatari kiasi cha kumfanya Zitto, ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi
kuhongwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa
Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao
makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu
ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
“Zitto anajua kuwa Andrea Cordes
aliniandikia baruapepe na nakala kwake nikawajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa
na makao makuu ya chama na tukipokea malalamiko rasmi tutachunguza kwa sasa
chama kinaichukulia ripoti hiyo kama ripoti nyingine zinazosambazwa
mitandaoni,” alifafanua Mnyika.
Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo,
Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa na
malalamiko.
Alisema baada ya taarifa hiyo ya siri
kusambaa mtandaoni, Zitto alitoa kauli na kama Dk Mkumbo hakuridhika, alipaswa
kuonana na watu wa Idara ya Uenezi ya Chadema.
“Idara
ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika
masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema Mnyika.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment