Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba
wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili achukue
mikoba ya Abdalla Kibadeni.
SIMBA itaanza mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu Bara, Januari 26 mwakani dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam ikiwa na kocha mpya, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha.
Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba
wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili achukue
mikoba ya Abdalla Kibadeni.
Williamson (52), ni straika wa zamani
wa West Bromwich Albion na katika mechi 53 aliyoichezea timu hiyo alifunga
mabao 11.
Williamson, ambaye ni raia wa
Scotland alijiunga na Gor Mahia msimu huu na tayari ameipa ubingwa wa Ligi Kuu
Kenya ikiwa ni miaka 18 tangu timu hiyo itwae ubingwa wa Kenya mwaka 1995.
Williamson, ambaye alikuwa kocha wa
timu ya taifa ya Uganda na kuipa ubingwa wa Kombe la Chalenji mara nne, ni
kocha anayesifika kutokana na kufundisha soka la kisasa kwa timu kushambulia na
kukaba kwa pamoja.
Habari kutoka makao makuu ya Simba,
barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam zinasema kuwa maofisa kadhaa wa klabu
hiyo wameanza mazungumzo na kocha huyo.
Habari hizo zinasema kuwa Simba ina
asilimia kubwa ya kumnasa kocha huyo kwa sababu alikuwa na mkataba wa mwaka
mmoja tu Gor Mahia na kwamba analipwa kidogo.
Simba imeamua kuingiza nguvu zake kwa
kocha huyo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo ambayo inashika
nafasi ya nne katika ligi, lakini kubwa zaidi ni kutokana na benchi la ufundi
kushindwa kudhibiti nidhamu kwa wachezaji na kucheza mpira wa hovyo uwanjani.
Hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa
tayari kulizungumzia hilo, licha ya karibu wote kukiri kuwa hawaridhishwi na
jinsi timu hiyo inavyocheza.
Williamson aliteuliwa na Shirikisho
la Soka Uganda (Fufa) kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo 'The Cranes'
Agosti 19, 2008 akichukua nafasi ya Csaba Laszlo, aliyekuwa amejiuzulu Julai
2008 baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Hearts inayoshiriki Ligi Kuu
Scotland.
Akiwa na kikosi cha Uganda,
Williamson ameshinda mataji manne ya Kombe la Chalenji mwaka 2008, 2009, 2011
na 2012.
Uganda nusura itinge katika fainali
za Mataifa ya Afrika 2013, lakini ilipoteza mchezo wake wa mwisho wa kufuzu
baada ya kupigiana penalti na Zambia.
Hata hivyo, Fufa ilimtimua kazi
Williamson Aprili 8, mwaka huu na nafasi yake ikachukuliwa na Kocha wa Serbia
Sredojevic Milutin 'Micho', ambaye alikuwa ametimuliwa timu ya taifa ya Rwanda.
Julai 5, mwaka huu, Williamson
alijiunga na Gor Mahia ya Kenya akichukua nafasi ya Zdravko Logarusic wa
Croatia, ambaye alikuwa amefukuzwa siku tisa za nyuma yaani Juni 25 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment