na Josephat Isango
HOFU ya kung’oka kwa mawaziri
wasiopungua watano akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imeanza kushika kasi
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba,
huenda safari hii usiwe upepo unaopita tu bila madhara, bali kikawa kimbunga
cha kuwaondoa madarakani mawaziri hao kwa madai ya kushindwa kuwajibika.
Pinda na mawaziri wenzake, Emmanuel
Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi),
Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa) wanashinikizwa kujiuzulu.
Mawaziri hao juzi walishambuliwa na
wabunge kuwa taasisi na watendaji walio chini yao wameendesha operesheni za
kupambana na ujangili na kuhamisha mifugo zilizosababisha vifo, ubakaji,
majeruhi na uharibifu wa mali kwa wananchi wasio na hatia.
Tayari Bunge limepitisha azimio la
kuunda kamati teule ambayo inatarajiwa kutangazwa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda, bungeni kesho.
Hatua ya kuundwa kwa kamati teule ya
Bunge kumekitia hofu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho tangu mwaka 2008
kimekuwa kikihaha kutibu majeraha ya makundi yanayohasimiana yanayodaiwa
kushamiri mara baada ya Edward Lowassa kujiuzulu.
Majina ya kamati teule yanayotarajia
kutangazwa kesho, ndiyo yatakayotoa picha ya mwelekeo wa siasa za chama hicho.
Iwapo kamati teule ikibaini tuhuma
walizotoa wabunge, za watu kubakwa, kuuawa, kuteswa, ng’ombe kupigwa
risasi, wafugaji kutozwa faini kubwa, kulazimishwa kuuza mifugo yao kwa bei
ndogo, Pinda na mawaziri wenzake waliotajwa watalazimika kujiuzulu au rais
kutengua uteuzi wao.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanadokeza
kuwa kuendelea kuwapo madarakani kwa Pinda kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na
Rais Jakaya Kikwete, ambaye mara kwa mara amekuwa akimkingia kifua licha ya
kupelekewa malalamiko ya utendaji hafifu wa Pinda.
Baadhi ya makada waliozungumza na
Tanzania Daima Jumapili, wamedokeza kuwa kitendo cha wabunge kuunda kamati teule
ya kuchunguza migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hakitamnusuru
Pinda.
Makada hao wanasema Pinda hawezi
kuepuka kimbunga hicho kwa madai kuwa baadhi ya wabunge na hata mawaziri
hawaridhishwi na utendaji wake, hivyo matokeo ya tume hiyo yatatoa fursa ya
azima yao ya siku nyingi ya kutaka kumng’oa madarakani.
Rais Kikwete ndiye tegemeo pekee la
kusalia madarakani kwa Pinda anayedaiwa kushindwa kuimudu ofisi hiyo iliyoachwa
na mtangulizi wake, Lowassa, aliyejiuzulu Februari mwaka 2008, baada ya kuguswa
na kashfa ya Richmond.
Historia ya kamati inaonyesha kuwa
ripoti zake mara nyingi zimesababisha kujiuzulu au kuondolewa madarakani kwa
watu wanaoguswa nazo.
Mtangulizi wa Pinda ambaye ni Mbunge
wa Monduli, Lowassa, alilazimika kuondoka madarakani baada ya ripoti ya kamati
teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, kubaini kulikuwa na
upendeleo katika zabuni iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond.
Pinda inadaiwa amekuwa si mtoaji
maamuzi kwa masuala yanayowagusa watendaji walio chini yake, hivyo kuathiri
utendaji kazi wa serikali.
Kama Pinda atajiuzulu, Rais Kikwete
atalazimika kuunda baraza jipya la mawaziri ambalo litakuwa la nne tangu aingie
madarakani mwaka 2005.
Rais Kikwete aliunda serikali mwaka
2006 mara baada ya kuingia madarakani lakini Aprili 2008 alifanya mabadiliko
baada ya Lowassa kutuhumiwa na kamati teule iliyoundwa kuchunguza kashfa
mbalimbali zilizohusu kampuni za kuzalisha umeme.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 Rais
Kikwete alifanya mabadiliko kwa mara ya pili, baada ya kuchaguliwa tena kwa
awamu ya pili, huku waliokuwa mawaziri 2005-2010 wakiangushwa katika
kinyang’aro cha ubunge kwenye majimbo yao.
Kikwete alifanya mabadiliko mengine
Mei mwaka jana, mabadiliko yaliyomwacha aliyekuwa Waziri wa Fedha Mustapha
Mukulo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara, Cyril Chami, aliyekuwa Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda na
aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Waziri mmoja wa zamani anasema
wabunge watakaoteuliwa na Spika kuunda kamati teule wanaweza kutumia mwanya wa
makundi ya kisiasa kumwajibisha Pinda na wenzake kwa lengo la kujiimarisha kwa
ajili ya uchaguzi wa rais mwaka 2015.
Historia za kamati teule
Historia inaonyesha kuwa kila kamati
teule ilipoundwa haikuwaacha salama watuhumiwa, ikiwa ushahidi utatolewa wa
kutosha. Juzi Spika Makinda aliafiki wazo la kuundwa kwa kamati teule.
Hata hivyo kamati teule hizo kila
zinapoundwa na ripoti yake kusomwa zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani
kwa watendaji mbalimbali.
Februari 8, 2008, Waziri Mkuu, Edward
Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya kamati teule iliyoundwa na Bunge
kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya
Richmond kumgusa.
Mwaka juzi, Bunge liliunda kamati
teule kuchunguza matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa
kuchangisha sh milioni 50 kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara, ili
kufanikisha upitishwaji wa bajeti, na ripoti yake ilimng’oa Katibu wake, David
Jairo.
Mvutano
Wakati hofu hiyo ikitanda Bunge
limegawanyika katika suala hili, kukiwapo mvutano mkubwa kama mawaziri hao
wawajibishwe au la, licha ya mawaziri hao kutoa kauli za serikali na kuomba
radhi ili wahusika waweze kuwajibishwa.
Tayari Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola (CCM), amejitokeza na kusema hoja yao imetekwa na Spika wa Bunge,
Makinda, na kuifanya ni ya kwake na si ya wabunge waliotoa hoja.
“Hoja imechukuliwa na Spika, akaanza
kuamua baadhi ya mambo yaanze kuchunguzwa na Kamati ya Kudumu ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira, ambayo imeteuliwa na yeye, tulitegemea tupewe fursa ya
kuhitimisha hoja zetu kisha iundwe kamati teule kutegemea hadidu za rejea
za wabunge, lakini kwa utaratibu uliofuatwa na Spika, watoa hoja hatujapewa
nafasi ya kuhitimisha hoja zetu,” alilalamika Lugola.
Lugola aliongeza kwamba damu
zilizomwagika hazitaenda bure, watu wakileta majibu mepesi yasiyowawajibisha
Pinda na wenzake hatakubali, maana wananchi wameuawa, wamebakwa, wameteswa,
ng’ombe wakauawa kwa kupigwa risasi, kama kuna mbunge asiyewapenda Watanzania
apeleke utetezi kwa masuala hayo mazito.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM)
alisema kila chama kilichoko madarakani kinapenda kutawala, hivyo mawaziri
waliozembea iwapo hawatachukuliwa hatua chama kinachoongoza kinajiandalia
anguko katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo baadhi ya wabunge wa chama
tawala wanaona haikuwa busara kwa Spika Makinda kuruhusu hoja ya kuundwa kwa
kamati teule, hasa katika kipindi hiki ambapo vyama vya upinzani vimeonekana
kuimarika zaidi.
Kuimarika kwa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi kumechangia makada wa CCM kujawa na hofu ya kile
kitakachogunduliwa na kamati teule.
Wabunge hao walisema hivi sasa bado
chama chao hakijapata uungwaji mkono katika mchakato wa sheria ya Katiba mpya, hivyo
kamati teule inaweza kuongeza utete ndani ya serikali na CCM.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment