Friday, November 1, 2013

MFADHILI WA UGAIDI MBARONI



Jeshi la Polisi, Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, limemkamata mfanyabiashara wilayani humo, Bw. Juma Kheri maarufu kwa jina la 'Chifu Abiola', akituhumiwa kufadhili kikundi cha kigaidi kilichokuwa na kambi tatu Kata za Lwande na Negero.

Akizungumza na Majira, Mjini Songe, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Suleiman Liwowa alisema Bw. Kheri alikamatwa siku tatu zilizopita na yupo mahabusu wilayani Handeni.
Hata hivyo, Bw. Kheri alipekuliwa katika nyumba anayoishi, duka la jumla na nyumba ya kulala wageni kuanzia 8:30 mchana hadi saa 12.30 jioni.

Bw. Liwowa alisema polisi walipata shida kubaini jina lake halisi, kwani alikuwa anatambulika kwa majina ya Juma Sahel, lakini baadaye wakabaini anaitwa Juma Abdallah Kheri.

"Hadi sasa bado anashikiliwa polisi Mjini Handeni, watu walikuwa wakimjua kwa majina mengine lakini hivi sasa jina lake halisi libebainika," alisema Bw. Liwowa.
Alisema watu wengine wanaohusishwa na vitendo vya ugaidi wamekamatwa kwenye Kijiji cha Gombero, Kata ya Kibirashi wilayani humo.

Aliwaomba wakazi wa Wilaya hiyo,wasiwachukie waumini wa dhehebu la Ansaar Sunna kwani si wahalifu bali waliokuwa wanafanya vitendo vya kigaidi ndiyo wahalifu.
"Serikali haipambani na Ansaar Sunna, bali wahalifu, sisi tunaheshimu dini zote hivyo mnapowaona waumini hao msije mkawafanyia vitendo vibaya," alisema Bw. Liwowa.
Aliongeza kuwa , awali hawakujua kama kundi lilo ni tishio lakini tangu wameanza kupambana nalo, wamebaini ukweli na nguvu yao ni kubwa.

Bw. Liwowa alisema hadi sasa kikundi hicho kimeweza kusambaratishwa lakini polisi bado wameweka kambi kwenye Kata za Negero na Lwande.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, alisema kundi hilo ambalo lilikuwa likifanya vitendo vya ugaidi katika Kata za Lwande na Negero, lisihusishwe na dini ya Kiislamu bali hao ni magaidi, majasusi na wanatakiwa kulaaniwa na kupingwa.

"Lile ni kundi la kigaidi si wahalifu wa kawaida, lakini naomba lisihusishwe na dini ya Kiislamu, sisi sote tunafahamu hakuna dini inayoruhusu vitendo vya ugaidi, kuvuruga amani," alisema
Chanzo: Majira

No comments: