Serikali ya Zimbabwe, imetia saini mkataba na benki ya
serikali ya China kuinua hadhi ya mradi wake wa kuzalisha kawi ya maji katika
bwawa la maji la Kariba.
Waziri wa fedha wa Zimbabwe, Patrick Chinamasa, alisema kuwa
benki hiyo hutoa mkopo wa takriban dola milioni tatu hadi ishirini kwa mradi
huo ambao utasaidia kumaliza tatizo la uhaba wa umeme huku serikali ya China
nayo ikitoa ufadhili wa ziada.
Zimbabwe imekuwa ikiimarisha uhusiano wake na China hasa
baada ya Marekani na Ulaya kuiwekea nchi hiyo vikwazo.
Waziri Chinamasa alisema kuwa mkopo huo utalipwa na Zimbabwe
pamopja na riba ya asilimia mbili kila mwaka kwa miaka ya kwanza tano na kisha
kulipa mkopo utakaosalia kwa miaka 20.
Pesa hizo zitatumiwa kuongeza uwezo wa bwawa la kuzalisha
kawi ya maji kwa megawati 300.
Zimbabwe huzalisha kawi yenye megawati 1,200 kwa kawaida
kila siku ikilinganishwa na mahitaji ya megawati 2,100 kila siku.
Ili kukabiliana na uhaba wa umeme wakati mahitaji ni
makubwa, baadhi ya sehemu za mji husalia bila umeme kwa hadi masaa kumi hususan
katika miji mikubwa.
Zimbabwe imeendelea kuimarisha uhusiano wake na China baada
ya kutofautiana na nchi za Magharibi.
Marekani na Ulaya ziliiwekea nchi hiyo vikwazo, ikiwemo vya
usafiri pamoja na kupiga tanji mali zake Rais Robert Mugabe na washirika wake
baada ya uchaguzi wa mwaka 2002, ambao waangalizi wa Ulaya walisema ulikumbwa
na visa vya wizi wa kura na kwamba Mugabe hakushinda kwa njia halali.
No comments:
Post a Comment