Dodoma. Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba
(CCM), amemshukia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kuwa
amebeza kauli ya Bunge na kukejeli chombo hicho kwa kwenda kuzungumzia
Operesheni Tokomeza Majangili nje ya Bunge, wakati uamuzi ulishatolewa bungeni.
Mkumba, jana aliomba mwongozo wa
Spika kupitia kanuni ya 68 na hatua hiyo aliifanya muda mfupi baada ya
kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Mbunge huyo alisema juzi wabunge
walijadili kwa kina hoja ya dharura kuhusu maonevu wanayofanyiwa wananchi
katika Operesheni Tokomeza Majangili.
Alisema hata hivyo Balozi Kagasheki,
ameonekana na kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wabunge wanasema
sema tu ndani ya Bunge lakini hawajali rasilimali za taifa.
Alisema waziri huyo pia alisema
hatishwi na uamuzi ya wabunge wa kumtaka ajiuzulu na kwamba hatoki hadi
aliyemteua abatilishe uamuzi wa uteuzi wake.
“Sasa kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye
aliyetoa kauli ya kusitisha operesheni hii ya Tokomeza na kitendo cha
kuwakamata Wachina ni zoezi tu la Serikali la kila siku ambalo linaweza
kuendelea bila operesheni,” alisema.
Je, mheshimiwa Spika, mheshimiwa
waziri aliyetoa kauli ndani ya Bunge na anatoka nje na anabeza kauli ya Bunge,
anakejeli Bunge naomba mwongozo wako kama jambo hili linaruhusiwa, “ alisema
mbunge huyo.
Spika Makinda aliwaonya wabunge na
mawaziri kutotumia vibaya midomo yao.
“Nadhani matumizi mabaya ya mdomo
yasitumike kwa sababu tukishakubaliana vitu hapa kwenda kusema vitu vingine ni
kuwasha moto pengine uliokuwa unaendelea kuwaka vizuri,”alisema.
Bunge liliazimia kuunda kamati
maalumu ya kuchunguza operesheni hiyo ambapo Spika Makinda aliahidi kutangaza
wabunge watakaounda kamati hiyo jana.
Akizungumza baada kukamata pembe 706
za ndovu jijini Dar es Salaam, Balozi Kagasheki alisema wabunge wanaomtaka
ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya
watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya
Kikwete pekee.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na
baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya
kisiasa.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment