Meya mpya wa New York Bill de Blasio na familia yake wakisherehekea ushindi.
Chama cha Democrat nchini Marekani
kimeshinda uchaguzi katika majimbo ya New York na Virginia, ambayo yalikuwa
yakiongozwa na warepublican. Chama cha Republican kilishinda uchaguzi mwingine
katika jimbo la New Jersey.
Meya mpya wa New York Bill de Blasio
na familia yake wakisherehekea ushindi.
Uchaguzi huo wa jana ni wa kwanza
mkubwa kufanyika nchini Marekani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2012, ambao
rais Barack Obama alishinda na kupata muhula wa pili madarakani.
Katika jiji kubwa zaidi nchini humo,
New York, mwanasiasa mwenye msimamo wa kiliberali Bill de Blasio alishinda
uchaguzi kwa tiketi ya chama cha Democrat, akimshinda kwa mbali mpinzani wake
Joe Lhota wa chama cha Republican, na kuwa meya wa kwanza mdemocrat kupewa
ufunguo wa jumba la meya wa New York tangu mwaka 1989.
Uchaguzi mwingine muhimu ulikuwa
katika jimbo la Virginia ambalo kawaida ni ngome ya chama cha Republican lakini
baada ya ushindani mkali. Terry McAuliffe alitangazwa mshindi katika
kinyang'anyiro cha ugavana, dhidi ya Ken Cuccineli wa chama cha Republican
aliyekuwa mwanasheria mkuu wa jimbo hilo.
New Jersey yabakia kwa warepublican
Chama cha Republican hakikuambulia
patupu. Mgombea wake wa ugavana katika jimbo la New Jersey, Chris Christie
alimshinda kwa kishindo mpinzani wake wa chama cha Democrat Barbara Buono.
Chama cha Democrat pia kilipata
ushindi katika mji uliofilisika wa Detroit, na katika mji wa Boston.
Na katika jimbo la Virginia, mfumo wa
wakazi wake uliokuwa wa wanavijiji wenye mrengo wa kihafidhina unabadilika na
kuwa wa miji yenye maoni ya kiliberali, uchaguzi huu pia ulikuwa kipimo cha
namna kura itakavyopigwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.
Muundo wa wakazi wa jimbo hilo
umebadilishwa na kuongezeka kwa wakazi ambao ni wafanyakazi wa serrikali na
wanajeshi.
Kitisho kwa mahafidhina
Ushindi wa Chris Christie katika
jimbo la New Jersey, sambamba na kushindwa kwa mwenzake wa jimbo la Virginia
Ken Cuccineli, unaweza kuimarisha dhana kwamba pengine chama cha Republican
kinapaswa kuwatenga wagombea wake wenye misimamo mikali ya kihafidhina.
Kushindwa kwa Cuccineli hasa
kunachukuliwa kama kipigo kikubwa kwa kundi la Tea Party lenye mrengo mkali wa
kulia katika chama cha Republican, ambalo katika uchaguzi wa mwaka 2010
lilifanikiwa kuwaingiza wajumbe wengi katika bunge mjini Washington.
Rais Barack Obama aliwapigia simu
washindi wa chama cha Democrat na kuwapongeza. Ushindi huo, hususan katika jiji
la New York unatazamwa kama wezani wa maoni ya umma huku uchaguzi wa bunge wa
katikati mwa muhula utakaofanyika mwaka 2014 ukibisha hodi.
Hata hivyo wapo wachambuzi
wasiokubaliana na maoni hayo, wakisema yaliyotokea katika majimbo ya Virginia
na New Jersey hayawezi kutabiri yatakayojiri katika uchaguzi wa wabunge na
magavana katika sehemu nyingine za nchi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/Reuters
Mhariri:Hamidou Oummilkheir
No comments:
Post a Comment