• Wengi
wafeli Hisabati, waongoza Kiswahili
na Happiness Mnale
KIWANGO cha ufaulu katika matokeo ya
darasa la saba mwaka huu kimeongezeka, ambapo wanafunzi 427,606, sawa na
ongezeko la asilimia 19.89 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika
shule za sekondari za serikali.
Hata hivyo licha ya ufaulu
kuongezeka, matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefeli somo la
Hisabati na wamefanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini
Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Dk. Charles Msonde,
alisema somo la Kiswahili liliongoza kwa asilimia 69.06 huku Hisabati
likiambulia asilimia 28.62.
Alisema kwa upande wa somo la
Kiingereza, lilifanya vizuri kwa asilimia 35.52, Maarifa ya Jamii asilimia
53.00 na Sayansi asilimia 47.49.
Katika hatua nyingine, wavulana
wameng’ara kwa kuongoza kwa asilimia 55.1 na kuwapita wasichana waliopata
asilimia 46.68.
Alisema wanafunzi 427,606
wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Alisema kati ya wanafunzi hao,
wasichana ni 208,227 na wavulana ni 219,379, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi
waliochaguliwa kuongezeka kwa asilimia 19.89 tofauti na mwaka jana ambapo
kiwango kilikuwa asilimia 8.8 .
Dk. Msonde alisema kuwa mtihani huo ulifanyika
Septemba 11 na 12 ambapo watahiniwa walitumia karatasi maalumu za ‘optical mark
reader’ na kusahihishwa kwa mfumo wa kompyuta.
“Matokeo haya yanaonyesha kuwa jumla
ya watahiniwa 9,126 walipata daraja A, wakati wanafunzi 82,293 walipata
daraja B.
“Jumla ya wanafunzi 336,187 walipata
daraja C, 389,948 daraja D na waliobaki, yaani 27,367 walipata daraja E,”
alisema Msonde.
Hata hivyo, Msonde, hakuweza kutaja
mikoa iliyofanya vema na ile iliyoshika nafasi ya mwisho, zikiwamo shule
zilizoongoza na kueleza kuwa baraza limewasilisha matokeo hayo kwenye mamlaka
husika.
“Tumewasilisha matokeo kwa mamlaka
husika ili zifanye uchaguzi wa watahiniwa wa kujiunga na elimu ya sekondari na
matokeo hayo yatatangazwa na mamlaka husika mara baada ya kazi ya uchaguzi
itakapokamilika,” alisema.
Akizungumzia udanganyifu katika
mtihani, alisema takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa
matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema waliofutiwa matokeo mwaka huu
ni watahiniwa 13, ikilinganishwa na watahiniwa 293 waliofutiwa matokeo kwa
undanganyifu mwaka jana.
Kuhusu tatizo la baadhi ya wanafunzi
kutojua kusoma na kuandika, Msonde alisema ni mapema mno kulijua hilo, kwani
linahitaji muda.
Wanafunzi 844,983 wa shule za msingi
walisajiliwa kufanya mtihani huo wa kumaliza darasa la saba, wengine 23,045
sawa na asilimia 2.66 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya
utoro, vifo, ugonjwa na wasichana kupata mimba.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment