na Mwandishi wetu
SIKU tatu baada ya serikali kutangaza
mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu, licha ya kupingwa na wengi, kitendo hicho pia
kimemhuzunisha Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk.
Slaa alisema: “Kwa kubadili mfumo wa maksi serikali sasa bila huruma
imeamua kwa makusudi kabisa kuua ubora wa elimu nchini, ni kweli kwa kupanua
wigo wa kufaulu serikali haitalaumiwa kwa akili ya kawaida, itaonekana
wamefaulu wote, lakini elimu haitawasaidia watoto wenyewe, haitawasaidia wazazi
wenyewe, na haitasaidia taifa letu. Tutapataje madaktari bora, tutapataje
wanasayansi, walimu au wahandisi bora? Mabadiliko yanahitajika kusaidia
taifa hili lisizikwe na watu wasio na huruma.”
Kwa upande wake, Dk. George Kahangwa,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akizungumza kupitia kipindi cha
‘Tuongee’ kinachorushwa na Star TV, alisema hatua ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Profesa Sifuni Mchome, kutangaza mageuzi hayo ni kuonesha
ni jinsi gani serikali imeshindwa kutatua mzizi wa tatizo la elimu
nchini na baadala yake inatapatapa kwa kuja na sera iliyoiacha kuitumia toka
mwaka 1995 iliyotumia alama hiyo ya 50 kwa 50 kwa Tanzania Bara na 40 kwa
60, kwa Visiwani Zanzibar ambapo safari hii imeamua kuitumia tena na kuiweka
wazi.
Dk. Kahangwa alisema serikali licha
ya kutoa tamko la kubadilisha daraja jipya huku ikikiri kuwa ilikuwa ikitoa alama
za kuanzia 75 hadi 100 ndio ufaulu wa alama ‘A’ na daraja la kwanza, pasipo
kuiweka wazi kwa muda mrefu, sasa wameamua kuiweka wazi, huku ni kuwaada
Watanzania kwa kutumia sera ambayo hazitekelezeki.
“Hili ni janga la elimu, huko nyuma
waliondoa ‘sifuri’ kwenye ufaulu na kuweka ‘feli’, leo hii wanakuja tena na
kuongezea daraja la tano na kuita ‘ufaulu hafifu au ufaulu usioridhisha’, huku
ni kucheza na masuala ya msingi katika taifa. Kuja mbele za umma na kutangaza
tena juu ya sera hiyo waliyoiacha kwa muda pasipokuitumia ni jinsi gani sera
hiyo haitekelezeki tena,” alisema Dk. Kahangwa.
Dk. Kahangwa amewaomba Watanzania na
wadau wa habari nchini kujitokeza kuwahoji wadau wa elimu kama walishirikishwa
kwenye kupitishwa kwa mabadiliko hayo.
Dk. Kahangwa alisema hivi
karibuni kuna shirika lilifanya utafiti wa shule za sekondari 100 ambapo shule
nne tu ndizo zinahesabika kama shule bora huku 96 zikihesabika kama makambi ya
shule.
Hata hivyo, Mhariri Mtendaji wa
gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo, aliyekuwapo kwenye mahojiano hayo
alifananisha kitendo cha serikali kupanga madaraja hayo kuwa ni sawa na kupanua
magoli ya uwanja ili kila mchezaji afunge, huku akiitaka serikali iwaombe radhi
wananchi kwa kuwa ilianza kutumia mfumo huo bila kuwaarifu.
Naye Mratibu wa Chama cha Waandishi
wa Habari mkoani Mwanza, Edwin Soko, alisema mabadiliko haya yaliyolenga
kuongeza idadi ya wahitimu bila kuangalia uzoefu, yamesababisha taifa kukosa
falsafa na Dira ya Taifa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment