Mjumbe wa amani Umoja wa Mataifa na
Jumuiya ya Kiarabu Lakhdar Brahimi amesema leo kuwa kongamano linalopangwa la
amani jijini Geneva ili kumaliza vita vya Syria huenda lisiandaliwe bila ya
ushiriki wa upinzani.
Wakati
akikamilisha ziara yake mjini Damascus, Lakhdar Brahimi alitoa wito kwa pande
zote mbili, serikali ya Syria na upinzani kuhudhuria mkutano unaopangwa wa
amani. Mjumbe huyo wa amani amesema kabla ya kurejea mjini Beirut, kuwa
mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuandaliwa baadaye mwezi huu jijini Geneva,
hayawezi kuendelea kama upinzani Syria utasusia.
Nayo
Urusi imesema inataraji kuwa mkutano huo wa amani utaandaliwa kabla ya
kumalizika mwaka huu, licha ya tofauti zilizopo na Marekani kuhusu uwakilishi
wa upinzani. Waziri Mkuu Dmitry Medvedev ameziomba pande zote katika mzozo wa
Syria kulegeza msimamo wakati akiushutumu upinzani kwa kumtaka Rais Bashar
al-Assad aondoke kama masharti ya kabla ya mazungumzo.
Ndege
za Israel zashambulia kambi ya jeshi la Syria Ndege za Israel zashambulia kambi
ya jeshi la Syria
Ombi
la Brahimi na Medvedev, limekuja saa chache tu baada ya maafisa kusema kuwa
Israel imefanya shambulizi la kutokea angani katika kituo kimoja cha jeshi la
Syria ili kusitisha usafirishaji wa silaha kwa kundi la Hezbollah. Kituo cha
televisheni cha Al- Arabiya kimesema kuwa Israel imeipiga kambi ya jeshi la
angani la Syria katika mkoa wa Latakia, wakati ikiyalenga makombora ya Urusi
yanayotumiwa katika mashambulizi ya ardhini yaliyokusudiwa kupewa kundi la
wanambambo wa Hezbollah.
Afisa wa Marekani amethibitisha kwa shirika la habari
la AFP kuwa “kulikuwa na shambulizi la Israel“ lakini hakutoa maelezo zaidi
kuhusu eneo na kilicholengwa, wakati nao maafisa wa Syria wakikataa kuzungumzia
habari hizo. Mwezi Mei, Israel ilifanya mashambulizi mawili ya kutokea angani
ndani ya Syria, na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel akasema mashambulizi
hayo mawili yalizilenga silaha zilizoundwa nchini Iran ambazo zilikusudiwa
kupewa Hezbollah.
Hayo
yanajiri wakati Shirika la Kupambana na Matumizi ya Silaha za Sumu likisema
kuwa silaha zote za sumu nchini Syria zimedhibitiwa. Msemaji wa shirika hilo
Michael Luhan amesema “silaha zote zimewekwa katika mifuko ambayo haiwezi
kupasuliwa“. Amesema kuna tani 1,000 ya sumu inayoweza kutengeneza silaha,
pamoja na tani 290 za silaha za sumu. Shirika hilo pia limesema vifaa vyote vya
kutengenezea silaha za sumu vimeteketezwa.
Wakaguzi
wana hadi leo kuzuru maeneo yote na kuharibu vifaa vyote vya kutengeneza silaha
za sumu kwa mujibu wa muda uliowekwa kwenye azimio la Shirika la OPCW na Umoja
wa Mataifa.Katika uwanja wa mapambano, jeshi la Syria limesema majeshi
yameutwaa mji wa Sfeira katika mkoa wa Aleppo baada ya kuuzingira kwa siku 27,
huku kukiwa na ripoti kuwa waasi wameondoka kabisa katika eneo hilo.
Mwandishi:
Bruce Amani/AFP
Mhariri:
Josephat Charo
No comments:
Post a Comment