Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry yuko
mashariki ya kati katika ziara inayonuia kuyapiga jeki mazungumzo kati ya
Israel na Palestina yanayoonekana kuyumbayumba
Kerry ambaye ndiye mpatanishi mkuu
kati ya Israel na Palestina amesema panda shuka zinazoshuhudiwa zinatarajiwa
kama katika mazungumzo yoyote yale, lakini ana imani kuwa vikwazo vilivyoko
vitakabiliwa na kuleta amani ya kudumu katika kanda hiyo ya mashariki ya kati.
Kerry aliyasema hayo leo mjini
Bethlehem alikokutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas,
baada ya mkutano na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Jerusalem.
Waziri huyo wa Marekani amesema ana
hakika kuwa licha ya matatizo, viongozi wote wawili wa mamlaka ya ndani ya
Palestina Abbas na wa Israel Netanyahu wana nia ya kuafikia ufumbuzi wa mzozo
huo.
Licha ya tamko hilo lililojaa
matumaini kutoka kwa Kerry, uhasama unazidi kutokota kati ya pande hizo mbili
husika.
Vuta nikuvute yazidi mashariki ya
kati
Huku Palestina hapo jana ikitishia
kujiondoa kutoka kwa mazungumzo kufuatia azma ya Isreal ya kuendelea na mpango
wa kujenga makaazi mapya ya walowezi katika eneo linalozozaniwa, Waziri mkuu wa
Israel amewashutumu wapalestina kwa kubuni mzozo usiokuwepo na kutatiza
mazungumzo.
Palestina imeghadhabishwa na
kuendelea kwa Israel kujenga makaazi mapya ya walowezi, jambo ambalo Netanyahu
anasisitiza halikuweko kama sharti kutoka kwa Palestina wakati mazungumzo hayo
yalipofufuliwa miezi mitatu iliyopita na badala yake, Palestina ilitaka
kuachiwa kwa wafungwa 104 ili ishawishike kurejea katika meza ya mazungumzo.
Kerry amesema leo kuwa msimamo wa
Marekani ni kuwa ujenzi wa Israel ni kinyume na sheria na kwamba Palestina
haikukubaliana na ujenzi huo tangu mwanzo.Hii ni mara ya kwanza kwa waziri wa
mambo ya nje wa Marekani kutamka msimamo wazi kuhusiana na suala hilo tete.
Pande zote zahimizwa kurejea katika
meza ya mazungumzo
Kerry amesema wamesalia na miezi sita
kuambatana na ratiba ya kukamilisha mazungumzo na kukubaliana; mpango
uliofikiwa mwezi Julai kuweza kupiga hatua zinazohitajika ili ifikapo Aprili
mwakani yawe yamekamilika.
Pande hizo mbili pia zinatofautiana
kuhusu hatma ya Jerusalem na bonde la Jordan ambayo ni asilimia 40 ya Ukingo wa
Magharibi ambako Israel inataka kuendelea kuweka majeshi yake huko hata baada
ya makubaliano ya amani iwapo yataafikiwa.
Abbas siku ya Jumatatu amesema
Palestina haitakubali kuachia hata milimita moja ya ardhi yake mashariki mwa
Jerusalem ambako kunatarajiwa kuwa makao makuu ya utawala ujao wa Palestina
wala kuruhusu bonde la Jordan kukaliwa kijeshi na Israel.
Mshauri wa Abbas, Nimr Hammas,
amedokeza kuwa Palestina haina nia ya kujiondoa katika mazungumzo lakini
akaongeza anatarajia Marekani kuchukua msimamo mkali kama uliochukuliwa na
Umoja wa Ulaya kupinga ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi na Israel na sio
kuegemea upande wowote katika mzozo huo.
Akiwa mjini Bethlehem, Kerry
ametangaza kuwa Marekani itatoa msaada zaidi wa dola milioni 75 kubuni nafasi
za ajira kwa Wapalestina na kuboresha mabarabara, mashule na miundo mbinu.
Akimaliza mazungumzo na Abbas, Kerry
anatarajiwa kurejea Jerusalem kwa mkutano na rais wa Israel, Shimon Peres, na
baadaye jioni kuwa na dhifa ya chakula na Netanyahu.
Hapo kesho anapanga kusafiri kuelekea
Jordan ambako anatarajiwa kukutana tena na Abbas kwa awamu nyingine ya
mazungumzo.
Mwandishi:Caro Robi/ap/dpa
Mhariri: Josephat Charo
Chanzo:
DWSwahili
No comments:
Post a Comment