Waziri wa mambo ya nchi za nje wa
Marekani John Kerry akiri udukuzi huenda ukawa umekwenda mbali sana, haya
yanajiri wakati bado mvutano unaendelea kati ya taifa hilo na mataifa ya ulaya
juu ya madai ya udukuzi
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa
Marekani John Kerry
Baada ya siku kumi za mvutano juu ya
udukuzi huo taarifa ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
ndio ya kwanza ya kukiri kuwa huenda ikawa maafisa wa Ujasusi wa Marekani
wamevuka mipaka katika suala hilo la udukuzi.
Kerry pia ametetea mpango huo na
kusema kwamba tangu kutokea kwa mashambulizi ya septemba 11 mwaka wa 2001
nchini Marekani, na mashambulizi mengine jijini London na Madrid, Marekani na
nchi nyengine ni lazima zisimame pamoja katika kuwadhibiti magaidi ambao nia
yao ni kuuwa watu na kushambulia idara za serikali.
Kerry amesema tangu mwaka huo
kumekuwa na uchunguzi wa mawasiliano na kukiri kwamba uchunguzi mwengine huenda
ulikuwa unavuka mipaka.
Hata hivyo Kerry hakutoa maelezo
yoyote juu ya tamko lake hilo, lakini akasema kwamba tukio ambalo kwa sasa
linaleta mvutano na washirika wake wa karibu kama Ujerumani halitarejelewa
tena.
Waziri huyo wa nchi za nje wa
Marekani licha ya kukiri kwamba huenda udukuzi unaofanywa ukawa unapita mipaka
pia amehakikisha kuwa hakuna mtu yoyote anayehujumiwa katika mpango huo wa
kukusanya habari.
Wiki hii Kansela wa Ujerumani Angela
Merkel alihamaki na kumuweka sawa Rais wa Marekani Barrack Obama kuhusu madai
kwamba maafisa wa Ujasusi wa Marekani wamekuwa wakichunguza mawasiliano yake ya
simu na kusema kwamba iwapo hilo litathibitishwa basi hii itaondoa imani ya
Ujerumani kwa Marekani.
Wabunge wa Ulaya wataka kujua zaidi
juu ya udukuzi
Siku ya Jumatano wiki hii kundi la
wabunge wa Ulaya walikuwa mjini Washington Marekani kutaka kujua zaidi juu ya uchunguzi
wa Marekani kwa washirika wake.
Huku hayo yakiarifiwa kamati ya
baraza la seneti inayohusika na masuala ya Ujasusi nchini Marekani ilipitisha
mswada hapo jana unaodhibiti kiwango cha kufanya uchunguzi kwa kutumia vyombo
vya elektroniki lakini ikakubali udukuzi huo kuendelezwa.
Katika mswada huo imekubalika
uchunguzi wa mawasiliano unaweza kufanyika kwa miaka mitano tu. Mswada huo
umepingwa vikali na kampuni za teknologia pamoja na makundi ya kiraia nchini
Marekani.
Wakati huo huo mbunge mmoja wa Ujerumani
amekutana na mfichua siri za kijasusi za Marekani Edward Snowden mjini Moscow,
na kusema mfanyakazi huyo wa zamani wa shirika la Ujasusi la NSA yuko tayari
kuja Ujerumani kusaidia katika uchunguzi wa udukuzi wa mawasiliano ya simu ya
mkononi ya Kansela Angela Merkel.
Hans-Christian Stroebele mbunge wa
upinzani wa chama cha walinzi wa mazingira ameliambia shirika la habari la
Ujerumani la ARD kwamba inaonekana Edward Snowden anajua mengi juu ya sakata
hiyo na kusema kuwa atatoa habari zaidi leo katika barua aliyoiandikia serikali
ya Ujerumani na mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani.
Bunge la Ujerumani hata hivyo
limepanga kufanya kikao maalum Novemba 18 kuzungumzia juu ya udukuzi huo huku
chama cha walinzi wa mazingira kikitaka mashahidi kama Edward Snowden kuitwa
kueleza wanachokijua juu ya udukuzi huo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu
No comments:
Post a Comment