Maelfu
ya wananchi wamelazimika kutoroka makwao kutokana na mapigano makali
yanayoendelea mpakani mwa DRC na Uganda
Mapigano makali yamezuka kati ya majeshi ya serikali ya
Congo na waasi wa M23 katika mpaka wa mashariki na taifa la Uganda.
Mapigano makali yameripotiwa kutokea wakati majeshi hayo ya
serikali yanapojaribu kuchukua udhibiti wa maeneo yaliosalia mikononi mwa waasi
wa M23.
Mwandishi wa BBC Issac Mumena aliyeko katika eneo hilo la
mpaka wa Uganda na DRC anasema kuwa mapigano hayo yamesababisha maelfu ya
wakimbizi kuvuka na kuingia nchini Uganda kutafuta usalama na matibabu kwa wale
waliojeruhiwa.
Waasi wa M23 mnamo siku ya Jumapili walitoa wito kwa
wapiganaji wao kusitisha vita ili kuruhusu mazungumzo ya amani kufanyika kati
ya viongozi wa kundi hilo na waasi hao.
Hata hivyo, kwa mujibu mwa mwandishi wa BBC hakuna dalili ya
kufanyika mazungumzo ya amani.
Anasema kuwa hali ni tete sana katika eneo la mpakani.
Inaarifiwa kuwa waasi hao wanaonekana kujibu vikali
mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi wa serikali na hali ni mbaya kuliko
siku za awali, na taarifa zinasema kuwa wanajeshi wanakaribia kushinda vita
vyao dhidi ya waasi hao.
Mapigano ya hivi sasa yanakuja baada ya wanajeshi wa
serikali kudhibiti baadhi ya miji iliyokuwa imetekwa na waasi hao baada ya
kuwafurusha.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment