Kesi ya Rais wa Misri aliyeondolewa
madarakani Mohamed Mursi imeanza tena baada ya kuahirishwa na jaji.Washtakiwa
14 walivuruga utaratibu wa kesi kwa mayowe yao dhidi ya mahakama katika chuo
cha mafunzo ya polisi Cairo.
Bendera ya Rais aliyepinduliwa
madarakani Mohamed Mursi na saluti ya vidole vinne ikipeperushwa na wafuasi
wake nje ya chuo cha polisi Cairo.(04.011.2013)
Haikuweza kufahamika mara moja kesi
hiyo itaendelea kuahirishwa hadi muda gani leo hii Jumatatu
(04.11.2013).Wapinzani wa serikali inayoungwa mkono na jeshi wanasema kesi hiyo
ni sehemu ya kampeni ya kukiangamiza chama chake cha Udugu wa Kiislamu na
kurudisha utawala wa mabavu.
Hadi tunaingia hewani haikuweza
kufahamika kesi hiyo itaahiriswa hadi muda gani.
Hii ni mara ya pili katika kipindi
cha kama miaka miwili hivi kwamba rais aliyepinduliwa madarakani anafikishwa mahakamani
nchini Misri taifa ambalo baadhi ya watu wanahofia kwamba linarudi tena kwenye
utawala wa mabavu.
Kushtakiwa kwa Mursi na wenzake 14
Waislamu wa itikadi kali kwa madai ya kuchochea mauaji ya umwagaji damu yumkini
kukazusha mapambano mengine kati ya wafuasi wake na polisi.
Wanakabiliwa na mashtaka ya kuchochea
ghasia zilizosababisha vifo vya takriban watu 12 katika mpambano nje ya Ikulu
ya rais hapo mwezi wa Disemba baada Mursi kuwakasirisha wapinzani wake na agizo
lake la kutanuwa madaraka yake.
Mamia wakusanyika nje ya mahakama
Mursi alikwenda kwenye jengo la
mahakama hiyo kutoka mahala kusikojulikana kwa kutumia helikopta.Kesi hiyo
inafanyika katika mahala pale pale ambapo rais wa zamani wa nchi hiyo hiyo
Hosni Mubarak amekuwa akijibu mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya
waandamanaji.
Mamia ya wafuasi wa Mursi
wamekusanyika nje ya jengo la mahakama kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi
huyo aliyeondolewa madarakani.Bango moja lilikuwa na maadishi "Matakwa ya
wananchi yamebakwa" ikimaanisha mapinduzi ya jeshi kufuatia maandamano ya
umma dhidi ya utawala wa Mursi.
Mmojawapo wa mawakili wa
wanaompendelea Mursi anayetagemewa kuwepo katika kesi hii leo hii amesema
mashtaka yanayomkabili Mursi hayana msingi.
Amesema "Hakuna ushahidi kwamba
Dakta Mursi ametenda uhalifu wa aina yoyote ile.Kesi yenye umbo la kisiasa
chini ya mazingira ya mapinduzi haiwezi kufanyika kwa uwazi na kuwa ya
haki."
Dhamira ya kesi yatiliwa mashaka
Mursi mwenyewe amedokeza kwamba
hatambui haki ya mahakama hiyo kumshtaki na hatoteuwa timu ya wanasheria
kumwakilisha.
Iwapo washtakiwa watapatikana na
hatia wanaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo au kifungo cha maisha gerezani.
Chama cha Udugu wa Kiislamu kimetowa
wito wa kufanyika kwa maandamano makubwa leo hii lakini ukubwa wa maandamano
hayo umepunguwa kutokana na kuwepo kwa ulinzi mkubwa wa polisi.
Shirika la haki za binaadamu la
kimataifa Amnesty International limesema kesi hiyo ni mtihani kwa serikali ya
Misri ambayo inapaswa kuendesha kesi itayozingatia haki kwa Mursi.
Hassiba Hadj Sahraoui naibu
mkurugenzi wa shirika hilo kwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesema
kushindwa kufanya hivyo kutazidi kutilia mashaka dhamira ya kesi hiyo.
Katika ziara ya kiongozi mwandamizi
kabisa kuwahi kufanywa nchini Misri na afisa wa serikali ya Marekani tokea
kupinduliwa kwa Mursi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia
ametowa wito kwa kesi kuwa na uwazi na za haki kwa wananachi wote wa Misri.
Serikali ya Misri inakiri kwamba njia
ya kuelekea demokrasia nchini Misiri imekuwa ngumu lakini mabadiliko sahihi ya
kisiasa yatafanyika.
Mwandishi:Mohamed Dahman/ Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu
Chanzo:
DWSwahili
No comments:
Post a Comment