Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Chama cha NCCR-Mageuzi, Dkt. Sengondo Mvungi, amejeruhiwa vibaya kwa mapanga na
watu wanaodhaniwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana.
Tukio
hilo limetokea nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni, Dar es
Salaam, saa sita usiku ambapo Dkt. Mvungi alipigwa mapanga sehemu mbalimbali za
mwili wake.
Akizungumzia
tukio hilo, Dkt. Natujwa Mvungi ambaye ni mtoto wa Dkt. Mvungi, alisema watu
hao walivamia nyumbani kwa baba yake wakati amelala usiku, kumtaka awape fedha
na aliposema hana, walianza kumcharanga mapanga mwilini.
Dkt,
Natujwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB),
alisema baba yake ameumizwa zaidi eneo la kichwani na amelazwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, Bw. James Mbatia, alisema Dkt.
Mvungi amelazwa katika Chumba cha Watu Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU),
katika hospitali hiyo.
Alisema
Dkt. Mvungi ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi UB, baada ya kujeruhiwa na watu hao,
alikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha, mkoani Pwani lakini hali yake
haikuwa nzuri hivyo alilazimika kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili.
"Tumesikitishwa
na tukio hili, baada ya kumvamia na kumjeruhi, watu hao waliiba simu, fedha na
kompyuta mpakato (Laptop), wakati watu hao wamevamia Dkt. Mvungi alikuwa
amelala, alifikishwa Muhimbili saa 10 alfajiri," alisema Bw. Mbatia.
Aliongeza
kuwa, watu hao wamemjeruhi vibaya na hali yake si nzuri sana hivyo madaktari
wanaendelea kumhudumia kwa kumpatia matibabu.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura, alikiri
kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa, hadi jana jioni msako mkali ulikuwa
ukiendelea ili kuhakikisha wahusika
wa
tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
"Ni
kweli tukio limetokea kama ulivyosikia...sisi kama Jeshi la Polisi tunaendelea
na msako mkali ili kuwakamata wahusika, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa
kuhusiana na tukio hili," alisema.
Dkt.
Mvungi aliwahi kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 kwa tiketi ya
NCCR-Mageuzi
Chanzo:
Majira
No comments:
Post a Comment