Watu
kadhaa wameshitakiwa nchini Zimbabwe kwa kumtusi Rais Robert Mugabe
Mahakama ya kikatiba nchini Zimbabwe
imebatilisha sheria inayosema kuwa ni uhalifu kumtusi Rais wa nchi.
‘‘Viongozi wa mashitaka hawapaswi
kuwa na tamaa sana ya kuwashitaki watu wanaomkosoa Rais Mugabe katika kumbi za
ulevi na maeneo mengine ya kijamii,’’ iliamua mahakama ya kikatiba.
Angalau watu 80 wameshitakiwa chini
ya sheria hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo mwezi Mei, mwanaharakati
Solomon Madzore alikamatwa baada ya kudaiwa kumuita Mugabe 'Punda
anayechechemaa.'
Alikanusha kosa la kumtusi Rais.
Chini ya kifungu cha 33 cha sheria ya
uhalifu nchini Zimbabwe, mtu anaweza kufungwa jela hadi mwaka mmoja au kutozwa
faini ya dola 100 kwa kumtusi Rais.
Sheria hiyo ilipingwa na watu kadha
nchini humo akiwemo mkaazi mmoja wa mji wa Bulawayo Kusini mwa nchi, Tendai
Danga, aliyekamatwa miaka miwili iliyopita kwa madai ya kumtusi Mugabe wakati
alipozozana na polisi ndani ya baa.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini
Harare, Brian Hungwe, majaji tisa waliotoa uamuzi huo, walikubaliana kwa kauli
moja kuwa sheria hiyo inahujumu uhuru wa kujieleza na kuifanya vigumu kwa
serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi wao.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilimpa
waziri wa sheria, Emmerson Mnangagwa hadi tarehe 20 Novemba kukata rufaa.
Mwezi Agosti mahakama ilimwachilia
huru mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 26 Takura Mufumisi, aliyeshitakiwa
kwa kuwa na nia ya kutumia bango la karatasi lenye picha ya Mugabe kama
karatasi ya kujipangusia chooni ndani ya baa moja.
Katika kura ya maamuzi iliyofanyika
mwezi Machi, wananchi walipitisha katiba mpya ambayo inawapa uhuru zaidi wa
kujieleza.
Watu wengi wamepongeza uamuzi wa
mahakama wakiamini kuwa sheria ilikuwa imemlinda rais dhidi ya kukosolewa.
Chanzo:
BCSwahili
No comments:
Post a Comment