Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye anasema ripoti
hiyo ya Benki ya Dunia imeshtua taasisi yake na imewasikitisha sana kwa kuwa
badala ya kupanda, Tanzania imeporomoka kwa nafasi 11. PICHA | MAKTABA
Na Mwandishi
Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kuporomoka kwa
nafasi 11 katika kuweka mazingira bora ya biashara na kuvutia wawekezaji
kimataifa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Sekta
Binafsi nchini (TPSF) Tanzania imeporomoka kutoka nafasi ya 134 mwaka 2013 hadi
nafasi ya 145 kati ya nchi 185 katika kuweka mazingira bora ya biashara ili
kuvutia uwekezaji ikiwa ya mwisho Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey
Simbeye alibainisha hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumzia ripoti ya
sasa ya Benki ya Dunia inayotolewa kila mwaka kuhusu mazingira bora ya
biashara.
“Ripoti hii imeishitua taasisi yetu
na imetusikitisha sana kwa sababu badala ya kupanda, tunashuka na safari hii
tumeshuka kwa nafasi 11 hali ambayo siyo nzuri kwa uchumi wa nchi,” alisema.
Benki hiyo inapima hali ya nchi ya
ufanyaji biashara kwa kuangalia viashiria vilivyowekwa kimataifa vikiwemo
utoaji wa vibali vya ujenzi.
Mkurugenzi huyo wa TPSF ameishauri
Serikali kuhakikisha inaongeza kasi ya kuweka mazingira bora ya ufanyaji
biashara ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuvutia uwekezaji zaidi.
“Serikali haina budi kuongeza kasi ya
kujenga mazingira bora ya biashara ili kuvutia uwekezaji na ina wajibu wa
kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara ili nchi isizidi kuporomoka kwenye
viashiria vya kimataifa.
Alisema katika kukabiliana hali hiyo
watendaji wa Serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa vitendo kwani mazingira bora
ya biashara ndiyo yanavutia uwekezaji na kukuza pato la taifa.
Ripoti hiyo inataja viashiria vingine
vya mazingira bora ya ufanyaji biashara kuwa ni pamoja na upatakanaji wa umeme,
kuandikisha rasilimali, upatikanaji mikopo, ulindaji wawekezaji, mifumo ya
ulipaji kodi, namna ya kufanya biashara za mipakani, kuingia mikataba, kufungua
na kufunga biashara na kuajiri wafanyakazi.
Ripoti inaonyesha viashiria hivyo
havijaweza kutekelezwa kwa kasi inayotakiwa na Serikali ili kuhakikisha
Tanzania inapanda kutoka pale ilipo.
Imetaja nchi nane bora Kusini mwa
Jangwa Sahara zinazofanya vizuri ni pamoja na Mauritius ya 20, Rwanda ya 32,
Afrika Kusini ya 41, Botswana ya 56, Ghana ya 67, Zambia ya 83, Morocco ya 87
na Namibia ya 98.
Alisistiza kuwa katika mpango wa
kufikia uchumi wa kati mwaka 2025, ni vyema jambo hili likawa katika vipaumbele
vya Serikali ili kuzidi kuvutia biashara na uwekazaji.
Alisema
Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 aliagiza kazi ifanyike na vikosi kazi viliundwa
ili kufikia vigezo hivyo, lakini kasi haijawa kubwa kutokana na wahusika
waliopewa dhamana hiyo kutotimiza vyema wajibu wao.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment