na Mwandishi wetu, Dodoma
WABUNGE wanaotumia nyaraka za siri za
serikali, Bunge au taasisi yoyote ya umma kulipua mabomu mbalimbali ndani na
nje ya Bunge, kuanzia sasa 'watakiona cha moto' iwapo watakutwa nazo.
Mbali na nyaraka hizo, pia
watakumbana na kibano iwapo watazomea au kufanya vurugu zitakazosababisha
kuahirishwa kwa shughuli za Bunge.
Vibano hivyo vinatokana na mwongozo
wa kanuni za maadili ya wabunge ambazo zinatarajiwa kupitishwa wakati wowote
kuanzia sasa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa
mbunge atakayekutwa na nyaraka za siri zinazohusu utendaji wa serikali bila
kibali cha mamlaka husika, atahesabika ametenda kosa na atachukuliwa hatua.
Chanzo kimoja kimelidokeza gazeti
hili kuwa kanuni hizo zinamzuia mbunge kutumia taarifa zozote atakazozipata kwa
wadhifa wake wakati akitekeleza shughuli za Bunge au kamati kwa ajili ya
kujinufaisha, kujipatia fedha au kujipatia umaarufu.
Pia inaelezwa kuwa mbunge haruhusiwi
kutoa taarifa zozote za siri za Bunge anazozifahamu bila idhini ya mamlaka
husika.
Tanzania Daima limeelezwa kuwa kanuni
hizo zinakataza mbunge kumtuhumu mwenzake kwa jambo lolote bila ya kuwa na
ushahidi.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na
Tanzania Daima, wamebainisha kuwa kanuni za maadili hayo zinalenga kuwaziba
midomo wanaonekana kutumia nyaraka mbalimbali kuibua madudu yanayofanywa na
serikali, taasisi au idara zilizopo chini yake.
Waliongeza kuwa kanuni hizo zina
lengo la kurejesha nyuma dhana ya Bunge kuisimamia serikali, na badala yake
zinajenga mazingira ya serikali kulimeza Bunge.
Walibainisha kuwa mwongozo wa kanuni
za maadili ya wabunge utaisaidia serikali iendelee na madudu yake ambayo katika
siku za hivi karibuni yamekuwa yakianikwa bungeni na wabunge mbalimbali.
“Bunge linataka kuingia kwenye
historia mbaya, yaani linajipa kazi ya kulinda uovu wa serikali, hii ni aibu
sana. Sisi hatutakubali kupitisha mambo haya, tunasubiri siku ya kuyajadili,”
alisema mmoja wa wabunge.
Chanzo kingine pia kimedokeza kuwa
kanuni za maadili ya wabunge pia zinawazuia wabunge kujihusisha na vitendo vya
udhalilishaji, unyanyasaji wa kijinsia baina yao au vitakavyowashushia hadhi
katika jamii.
Tanzania Daima, limedokezwa kuwa
wabunge hawataruhusiwa kujishirikisha na watu au vyombo binafsi kwa ajili ya
kujipatia maslahi ya kifedha au mali yoyote inayoweza kuathiri utendaji wa kazi
za Bunge.
Inasemekana baadhi ya mambo yaliyomo
kwenye kanuni hizo ni yale yanayotajwa kwenye sheria za nchi, ikiwemo viongozi
na watumishi wa umma kutoa tamko la mali walizonazo.
Jingine linalodaiwa kuwemo kwenye
kanuni hizo ni mbunge anapaswa kuepuka mgongano wa maslahi, vitendo vya rushwa,
kutokuwa na ubinafsi na kutopokea au kutoa zawadi kwa ajili ya kutekeleza
majukumu yake.
Kanuni hizo zinadaiwa kumlazimisha
mbunge kuweka wazi umiliki wa hisa kwenye kampuni, taasisi au asasi yoyote
inayosimamiwa na kamati za Bunge.
Mbunge huyo pia atatakiwa kutoa
taarifa kwa spika ili asipangwe kwenye kamati zinazosimamia taasisi hizo lengo
likiwa ni kuepusha mgongano wa kimaslahi.
Pia kanuni hizo zinamtaka mbunge
kushirikiana vyema na watumishi wa Ofisi ya Bunge, taasisi za umma,
waandishi wa habari, asasi zinazojitegemea na makundi mbalimbali kwenye jamii.
Kanuni hizo pia zinaweka wazi kwamba
uamuzi wowote ya vikao vya kamati ya uongozi utatolewa hadharani na spika au
afisa yeyote wa Bunge kwa idhini ya spika.
Tanzania Daima lilizungumza na Naibu
Spika Job Ndugai, juu ya kanuni hizo ambazo alisema bado hazijafikishwa bungeni
kwa uamuzi, lakini anazikaribisha kwa mikono miwili.
Ndugai alisema amefurahishwa na
kipengele kinachomtaka mbunge kuweka wazi umiliki wa hisa kwenye kampuni,
taasisi au asasi yoyote inayosimamiwa na kamati za Bunge.
“Hizo kanuni zitatusaidia sana kwani
kuna baadhi ya wabunge wamekuwa wakizizungumzia kampuni fulani kwa ubaya au
mema, lakini kumbe wanamiliki hisa, sasa tutawatambua,” alisema.
Ndugai aliongeza kanuni hizo
zikifikishwa bungeni zitajadiliwa kwa kina kama kuna vitu vya kuongeza au
kupunguza na baadae zitapitishwa na kuanza kutumika rasmi.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment