Dodoma. Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013 ambayo ilipitishwa
na Bunge katika mkutano uliopita, ilikuwa na kasoro nyingi ambazo zingekwaza
kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Kutokana na hali hiyo, Spika Makinda
ameliambia Mwananchi kuwa kulikuwa na ulazima wa kufanya marekebisho katika
sheria hiyo hata kama Rais Jakaya Kikwete asingekutana na vyama vya siasa na
kukubaliana kuleta marekebisho katika kikao cha Bunge kinachoendelea hivi sasa.
Licha ya Makinda kutokuwa tayari
kuweka wazi kasoro hizo, gazeti hili limebaini kuwa mambo hayo hayatofautiani
sana na yale yaliyobebwa kama ajenda na vyama vya upinzani vilipokutana na Rais
Kikwete, hivyo kuwezesha kuanza mchakato wa sheria hiyo kupitiwa upya.
“Labda nikwambie hivi katika muswada
ule uliopitishwa siwezi kusema kilitokea nini, lakini kimsingi kuna
administrative issues (masuala ya kiutawala) nyingi ambazo kama sheria ikibaki
ilivyo, hata Bunge la Katiba haliwezi siyo tu kufanya kazi, bali hata
kuitishwa,”alisema Makinda.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini
kuwa Ofisi ya Bunge tayari imewasilisha mapendekezo yake Serikalini ikiainisha
maeneo yapatayo kumi yenye kasoro zinazopaswa kufanyiwa kazi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah
alikiri kwamba ofisi yake imewasilisha mapendekezo yake Serikalini, lakini kama
ilivyokuwa kwa Makinda hakuwa tayari kuingia undani wa mapendekezo hayo.
Juzi Serikali ilikuwa ikifanya
majadiliano ya mwisho na wawakilishi wa vyama vyenye wabunge kuhusu marekebisho
yanayopaswa kufanywa katika sheria hiyo, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema muswada huo
ungewasilishwa jana kwa Katibu wa Bunge.
Dk Kashililah alisema walibaini
upungufu kwenye sheria hiyo baada ya muswada kupitishwa na Bunge Uchunguzi wa
Mwananchi umebaini kuwa Ofisi ya Bunge imefanya uchambuzi wa kina kuhusu
umuhimu wa kuendelea kuwapo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tofauti na uamuzi
wa awali wa kuvunjwa kwa tume hiyo.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment