Mbunge wa Mfenesini (CCM), Suleiman Nassib Omar akiweka
saini baada ya Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangala (kushoto) kuanza kukusanya
saini za wabunge kwenye ukumbi wa bunge jana akitafuta kuungwa mkono katika
hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda.PICHA NA EDWIN
MJWAHUZI
Na Neville
Meena na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma: Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema
hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge
wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja
za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka
bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo
kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema
sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda
katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana,
Dk Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge, akitafuta
kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka
kanuni.
Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla
ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew
Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni
zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni kamati hiyo ya
bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa
wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba
kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Miundombinu.
Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja
yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu
majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja
masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili
jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria
ya The National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda akijibu hoja hizo jana
alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati
hiyo ni mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo
lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.
“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge
linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha
wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala
utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo
kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo
ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati hii hata Serikali ilikuwa
haikubaliani na sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi
kubwa na kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri
utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu
halafu nikashindwa”.
Kuhusu posho, Spika aliungana na
kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya
Bajeti imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya
siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.
“Lazima walete maombi na waeleze kwa
nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi
nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa
mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema.
Kadhalika alizungumzia suala la
wabunge wengine kuteuliwa kuingia kwenye kamati ambazo si zao ambapo alisema,
suala hilo pia ni la kawaida kwani hata katika mjadala unaoendelea wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala ameongeza wajumbe wa ziada.
“Ninafanya hivyo kupanua wigo wa
mjadala na mara nyingi kwa mfano kwenye kamati yetu ya Katiba nimeongeza
wabunge wenye uelewa wa masuala ya sheria ili watusadie kufanya uchambuzi,
maana unaweza kukuta kwenye kamati, watu wenye utaalamu kuhusu suala husika ni
wachache. Kwa hiyo siyo kosa kwa mujibu wa Kanuni zetu,” alisema Makinda.
Ukusanyaji saini
Kwa upande wake Dk. Kingwangalla jana
alikuwa akiendelea na ukusanyaji wa saini za wabunge huku akisema kuwa
amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kupeleka bungeni hoja yake.
Ukusanyaji wa saini ulifanywa kwa
kupitia fomu maalumu na kutoa taarifa kwamba wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi,
wote wameshasaini katika fomu hizo.
Akizungumza jana katika viwanja vya
Bunge, Dk Kigwangallah, alisema wabunge wa Chadema, walimweleza kuwa watafanya
hivyo baada ya kukutana katika kikao cha pamoja.
Hata hivyo Kiongozi wa Upinzani
Bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikiri kusikia
taarifa hizo lakini akasema walikuwa bado hawajaketi kama kambi ili kuwa na
msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.
Jana asubuhi wakati wa kipindi cha
maswali na majibu, Dk. Kingwangalla alionekana akipita katika baadhi ya meza za
wabunge akiwashawishi kusaini fomu za kumuunga mkono.
Hadi jana mchana wabunge wa CCM, na
CUF wapatao 30 tayari walikuwa wamesaini fomu hizo, wakimuunga mkono mbunge
huyo.
Alipoulizwa ulazima wa kukusanya
saini za wabunge wakati kanuni hazimtaki kufanya hivyo alisema, hilo
linamwezesha kujua nguvu aliyonayo katika kumuunga mkono kuhusiana na suala
hilo.
Hoja zake
Katika taarifa ya kusudio lake ambalo
Mwananchi imebahatika kuliona, Dk. Kingwangalla alisema uteuzi wa Serukamba ni
kinyume na masharti ya kanuni ya 116(3) na (4).
Alisema Juni 27, 2013, wakati wa
kutunga sheria ya fedha, Spika aliagiza kwa mabavu kuwa wabunge wote wenye
majedwali ya mabadiliko waende kwenye kamati ya bajeti.
“Uamuzi huu wa Spika ni wa kidikteta
na unapingana na masharti ya kanuni ya 88 ya kanuni za kudumu za Bunge ambapo
kwa ufupi ni kwamba majedwali ya mabadiliko hujadiliwa bungeni wakati wa kamati
ya Bunge zima na huamuliwa kukubaliwa ama kukataliwa na Bunge zima na si kamati
yoyote ya Bunge,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya kuipa mamlaka
makubwa kamati hiyo ni kuondoa mantiki ya uwepo wa Bunge lilopewa mamlaka ya
kutunga sheria zote za nchi na Katiba ibara ya 63 (3) ( c) na (d ).
Pia alisema Spika Makinda amekuwa wa
kwanza kuvunja masharti ya kanuni anazopaswa kuzitilia nguvu kama
anavyoelekezwa na kanuni ya 5 (2). Amevunja pia kanuni na hivyo anastahili
kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa masharti ya kanuni hizi ili kukidhi
masharti ya Ibara ya 84 (7) (d) ya katiba ya kumwondoa madarakani.
Alitoa mfano wa hoja ya dharura
iliyotolewa wakati MV Skagit ilipozama Julai 18, 2012 na siku zilipowasilishwa
hoja mbili zinazohusiana na mauaji ya kwenye vurugu zinazohusu migogoro baina
ya jamii za wakulima na wafugaji na wanyang’anyi wa mali na unyanyasaji wa
wafugaji unaofanywa kwenye operesheni tokomeza ujangili.
Katika kuhitimisha taarifa hiyo, Dk
Kingwangalla alisema: “Ni maoni yangu binafsi na ya wabunge wengi wanaoniunga
mkono kuwa Spika wa Bunge Anne Makinda apumzishwe kazi kwa tuhuma nilizozitaja
hapo juu.”
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment