JANA serikali kwa mara nyingine
imetangaza matokeo ya darasa la saba na kutoa takwimu zinazoonyesha kiwango cha
ufaulu kwa wanafunzi hao kimeongezeka kikilinganishwa na mwaka jana.
Hata hivyo matokeo hayo yanaonyesha
kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wamefeli somo la Hisabati ambalo mwaka jana
lilifanywa kwa staili mpya ya kuchagua majibu, jambo ambalo lililalamikiwa na
wadau wa elimu kwamba linashusha kiwango cha elimu nchini.
Tumeyapokea matokeo hayo kwa mtazamo
hasi kwa sababu teknolojia iliyotumiwa katika kufanya mtihani inayojulikana
kama ‘Optical Mark Reader’, ambayo kila mtihani maswali yalikuwa ya
kuchagua, hatukubaliani nayo.
Mtihani wa darasa la saba ulifanyika
Septemba 11 na 12, ambapo watahiniwa walitumia karatasi maalumu za ‘Optical
Mark Reader’ na kusahihishwa kwa mfumo wa kompyuta.
Matokeo hayo yametangazwa jana huku
Watanzania wakiwa katika hoja ya kupinga utaratibu unaotumika kama vigezo vya
ufaulu wa kidato cha nne, ambapo sasa serikali imetangaza vigezo vipya ili kila
anayehudhuria darasani awe amefaulu.
Kwa sera hiyo mpya ya elimu, kwa sasa
hakuna daraja la sifuri, ila madaraja yameongezewa maksi kuwezesha wanafunzi
wengi zaidi wafaulu bila kuzingatia elimu bora inayohitajika kwenye jamii.
Tanzania Daima Jumapili tumeshangazwa
na utaratibu wa elimu unaofanywa na serikali.
Kimsingi tukiendelea kufanya siasa
katika elimu ni vigumu kuingia katika ushindani wa ajira na nchi nyingine hata
za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwenye uhusiano unaolegalega.
Watoto hawa waliotangaziwa matokeo
tunaambiwa kiwango cha ufaulu kimeongezeka, lakini Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza
la Mitihani nchini, Dk. Charles Mchonde, ameshindwa kujua kama waliofaulu
wanajua kusoma na kuandika au la!
Dk. Mchonde amesema kwa suala la
kujua idadi ya wanaojua kusoma na kuandika linahitaji muda kulifanyia utafiti.
Sisi tunahoji kauli hiyo ya kiongozi
wa serikali, ni muda gani wanahitaji kujua kama waliofaulu wanajua kusoma au
la?
Je, ikitokea waliochaguliwa hawajui
kusoma na kuandika, nini hatima yao kwenye shule za sekondari ambazo pia huko
serikali inatangaza ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tano bila kufeli?
Tumeingia katika kile kilichoitwa
matokeo makubwa sasa kwa mbinu mbaya, kuleta matokeo tusiyo na uhakika nayo,
huku wanafunzi wanapokwenda sekondari tunawaondolea uwezekano wa kufeli hata
kama hawajui ili waonekane tu wamefaulu hata kama hawana elimu bora, je, huku
ni kusaidia taifa?
Tunachokiona sisi, ni kuwa serikali
imechoka kuzomewa na wananchi kwa kutowajibika kwenye masuala ya elimu.
Serikali imeogopa shinikizo la maandamano ya wanafunzi na wazazi kuhusu elimu,
badala yake hata matokeo yameanza kutolewa yakiwa na athari za kisiasa.
Kutokana na matokeo yaliyotangazwa na
serikali kushindwa kubaini kama waliotangazwa kuwa wamefaulu wanajua kusoma na
kuandika, tunasema kuwa watoto hawa hawajafaulu ila wamefaulishwa kwa lengo la
kuogopa shinikizo la wananchi ili serikali iseme kuwa sera ya matokeo makubwa
sasa inafanya vema.
Sisi tunachelea kuwa tukiendelea
kufanya utani katika suala la elimu tutakuwa tunasogeza tatizo badala ya
kulikabili na kulitatua.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment