Jengo la Nkurumah Katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam,
(UDSM). Picha na Maktaba
Na Mwandishi
Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa katika hatua
za utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwenye elimu, imebainika
kuwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaohitimu, wanafanya udanganyifu
kwenye utafiti kwa kufanyiwa na watu wengine au kununua uliokwisha andikwa.
Kila mwanafunzi anayesomea shahada ya
kwanza, uzamili au uzamivu hutakiwa kufanya utafiti ikiwa ni sehemu ya vigezo
vya kukamilisha masomo yake.
Hata hivyo, Mwananchi imebaini kuwapo
kwa wanafunzi wengi wanaotumia mbinu mbalimbali za kuandika utafiti huo bila
kwenda maeneo husika.
Uchunguzi wetu uliofanyika kwa muda
mrefu kwenye vyuo mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa baadhi ya
wanafunzi huchukua tafiti za zamani na kuzinakili upya, huku wengine wakichukua
kutoka kwenye mitandao na kuzifanyia marekebisho kidogo ili zifanane na eneo
analotaka kufanyia utafiti huo.
Mtafiti Mwandamizi ESRF
Mtafiti Mwandamizi, Taasisi ya
Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk Donatila Kaino anasema ni asilimia 20 tu
ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu nchini, ndiyo wanaoweza kuandika utafiti
kwa ufasaha.
Anasema tatizo hilo linatokana na
mfumo wa elimu uliopo nchini ambao haumpi mwanafunzi nafasi ya kujifunza
kuandika utafiti tangu akiwa shule ya msingi.
“Tatizo kubwa walimu hawafundishi;
mtalaa siyo tatizo sana, kama walimu hawafundishi tangu shule za msingi hadi
sekondari unategemea nini?” anahoji.
Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu
Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bhalalusesa, anasema wanafunzi wanaosomea
ualimu ambao wamefanya utafiti wao kwa njia ya udanganyifu, wanaweza kukwamisha
mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa sababu hawatakuwa na uwezo
wa kitaaluma unaotarajiwa.
Anasema alipokuwa Mkuu wa Shule ya
Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walibaini kuwa baadhi ya wanafunzi
walikuwa wanafanyiwa tafiti hizo,
hivyo waliamua kuweka utaratibu wa kumhoji
kila mwanafunzi namna ambavyo alikusanya taarifa zake.
“Walikuwa wakishaandika proposal
(muhtasari) tuliwaita waje wao wenyewe waeleze, ingawa ilichukua muda mrefu
kuwahoji wanafunzi wote, tulilazimika kufanya hivyo. Tulimuuliza sababu
zilizomfanya aandike mada aliyoichagua,” anasema Bhalalusesa.
Anasisitiza kuwa utaratibu wa
kuhifadhi tafiti zote zinazofanywa na wanafunzi kwenye tovuti utasaidia
kuwadhibiti watu wasio waaminifu.
Katibu Mkuu
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome (pichani) anasema kuwa
watu wanaofanya biashara ya kuwafanyia utafiti wanafunzi wanaichafua sifa ya
elimu ya Tanzania.
“Hawa watu wanaifanya elimu ya
Tanzania ionekane ni duni wakati siyo kweli,” anasema Mchome.
Anabainisha kuwa biashara hiyo ni
haramu na kwamba njia pekee ya kuitokomeza ni kwa wananchi kutoa taarifa
zitakazowezesha wahusika kukamatwa.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa
wanafunzi wengi huandikia nyumbani kwao utafiti wao, badala ya kwenda sehemu
husika na hivyo kutoa matokeo ambayo hayafanani na eneo tajwa.
Wanafunzi waliohojiwa wanasema kiasi
kidogo cha fedha wanachopewa kwa ajili ya kufanyia utafiti, ndiyo sababu kubwa
ya wao kushindwa kwenda katika maeneo wanayotakiwa kufanyia utafiti.
Wanafunzi Chuo Kikuu Dodoma
Mwalimu Imani Msengezi aliyehitimu
Shahada ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka jana, anasema wao hawakufanya
utafiti kama ambavyo wanafanya wanafunzi wanaosomea fani nyingine. Badala yake
waliandika andiko (dissertation), ambalo waliandika wakiwa katika makundi.
“Kwa kweli sisi hatukufanya research
(utafiti), tulifanya dissertation, ambayo tulipewa tufanye kwenye makundi kama
assignment ya darasani,” anasema Msengezi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
mzazi mmoja ambaye pia ni mfanyakazi katika sekta ya elimu huko Iringa,
alielezea namna ambavyo mtoto wake aliandikiwa utafiti na mtu mwingine
aliyempata baada ya kushauriwa na mhadhiri wake.
Mzazi huyo ambaye hakupenda kutajwa
jina lake, anasema aliambiwa na mhadhiri aliyemsimamia mwanaye utafiti kuwa atoe
kiasi kidogo cha fedha ili amtafutie mtu atakayemwaandikia utafiti huo kwa kuwa
anashindwa kuiandika inavyotakiwa.
Anasema: “Kwa namna anavyoufahamu
uwezo mdogo wa mwanafunzi, ana uhakika kuwa hawezi kuandika utafiti utakaokidhi
vigezo vinavyotakiwa.
Muda unakwenda na alichoandika
hakieleweki, ni bora amtafutie mtu amsaidie kuiandika (research)… alisema siyo
gharama kubwa, ni fedha kidogo tu atatakiwa kutoa.”
Pia imebainika kuwa wanafunzi wengine
hutoa rushwa kwa wakufunzi wao wasio waaminifu ili kuweza kufanyiwa tafiti,
jambo ambalo huwafanya kujikuta kwenye wakati mgumu wanapoambiwa wayatolee
maelezo namna ambavyo walifanya utafiti huo.
Tahliso
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi
wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Donati Salla anasema uwezo mdogo
wa kitaaluma wa wanafunzi na changamoto za teknolojia zimechangia kushuka kwa
kiwango cha ufanyaji utafiti hapa nchini.
Anasema mitalaa ya vyuo vikuu
inatofautiana kwa kiasi kikubwa, hivyo kuwafanya baadhi ya wanafunzi kuwa na
ujuzi mkubwa huku wengine wakibaki na uelewa mdogo.
“Kwa mfano, sera ya elimu haijafanya
utafiti kuwa somo lenye heshima. Katika nchi nyingine utafiti ni somo
linalojitegemea, lakini hapa kwetu kuna vyuo wanafanya utafiti huku sehemu
nyingine wanafunzi wanaambiwa waandike project paper (miradi), hakuna uwiano,”
anasema Salla na kuongeza kuwa:
“Teknolojia nayo imeleta changamoto
mpya. Kuna baadhi ya wanafunzi wanategemea kunakili kutoka kwenye intaneti kila
kazi wanayoambiwa kufanya.”
Mhadhiri Chuo Kikuu Tumaini
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya
Umma cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam, Ajuaye Mdegela anasema
wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanashindwa kufanya utafiti kwa sababu hawataki
kutumia muda mwingi katika kusoma.
“Uwezo wa wanafunzi wa kuandika
utafiti unapungua kila mwaka, wamekuwa wavivu na wasiopenda kusoma.
Hapa kwetu mwaka huu wanafunzi wawili
hawatamaliza chuo kwa sababu wameshindwa kufanya utafiti,” anasema Mdegela.
Anafafanua kuwa siku hizi wanafunzi
wanasoma kwa ajili ya kufaulu mitihani kwa kukariri na kwamba wanashindwa
kufanya vizuri kwenye utafiti kwa sababu wanatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha
kuhusu mada husika na si vinginevyo.
Anaongeza: “Kwa mfano unakuta
mwanafunzi ameandika idadi ya watu 90 atakao wahoji kwenye muhtasi wa utafiti
wake, lakini anapokwenda kuiandika anaandika watu 50 tu ndiyo aliowahoji. Hili
ni tatizo kwa kuwa tofauti haipaswi kuzidi asilimia kumi,” anasema.
Pia alibainisha kwamba wakati
mwingine mwanafunzi anaweza kuandika taarifa zisizohusiana kabisa na mada
anayoitafiti. “Inavyoonekana ni kama vile amenakili kutoka sehemu fulani
akabandika huku.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Iringa, Esau Ntabindi anasema wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu siku hizi
wanashidwa kusoma vizuri kwa sababu hawako makini na masomo.
Akizungumzia udanganyifu katika
kuandika utafiti, Ntabindi anasema: “Kuna wakati unasoma utafiti aliuofanya
mwanafunzi halafu unajiuliza kama ni kweli yeye ndiye aliyefanya.”
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini
kuwepo kwa mtu mmoja eneo la Kinondoni A, jijini Dar es Salaam, ambaye kwa muda
mrefu amekuwa akiwafanyia utafiti wanafunzi wa vyuo vikuu kwa malipo ya kati ya
Sh 50,000 hadi Sh 100,000.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment