Shirika la kushughulikia wakimbizi la
Umoja wa Mataifa UNHCR limesema mzozo wa Syria umesababisha mzozo mkubwa zaidi
duniani wa wakimbizi kwani umesababisha zaidi ya raia milioni 9 wa Syria
kuachwa bila makaazi.
Kamishna mkuu wa shirika hilo la
UNHCR Antonio Guterres amesema asilimia 40 ya wasyria wameyatoroka makaazi yao
huku zaidi ya milioni 6.5 kati yao wakitafuta hifadhi salama ndani ya Syria
kwenyewe na wengine milioni 2.6 wakitorokea nchi jirani.
Guterres amesema ni jambo lisiloingia
akilini ni vipi janga kubwa la kibinadamu la kiwango cha namna hiyo linajiri
machoni mwa walimwengu bila ya hatua zozote za maana kuchukuliwa kuzuia
umwagikaji mkubwa wa damu unaoendela Syria.
UNHCR imesema wengi wa wakimbizi wa
Syria wamepata hifadhi katika nchi zisizo na utajiri mkubwa kama
Misri,Iraq,Jordan,Lebanon,Uturuki na hivyo imeathiri pakubwa uchumi na miundo
mbinu ya nchi hizo.
Chini ya asilimia nne ya wakimbizi wa
Syria wako Ulaya
Ni kiasi kidogo cha wakimbizi wa
Syria wameweza kutafuta hifadhi katika nchi za Ulaya kutokana na hatari ya
kuzifika nchi hizo kupitia safari za majini na pia kukumbwa na hata hatari
kubwa zaidi iwapo watanusirika ya kukataliwa na nchi hizo.
Guterres amesisitiza kutumika kwa
kila juhudi kutafuta amani Syria ili kupunguza dhiki na mateso ya raia wasio na
hatia waliojikuta katika mzozo huo na kulazimika kuyatoroka makaazi yao,jamii
zao,kazi zao na maisha yao ya kawaida.
Vita hivyo vya Syria ambavyo vilianza
mwezi Machi mwaka 2011 kama wimbi la uasi la kutaka kumg'oa madarakani Rais
Bashar Al Assad limesababisha vifo vya zaidi ya watu 140,000 na kuziathiri pia
nchi za kanda hiyo kutokana na mzigo wa kuwapokea wakimbizi.
Nchini Lebanon pekee idadi ya
wakimbizi wa Syria inaelekea kufika milioni moja huku ikitarajiwa kuongezeka
hadi milioni 1.6 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
UNHCR imezitaka nchi za Ulaya,Amerika
ya Kaskazini na Asia kutoa nafasi kwa wakimbizi wa Syria.
Bunge la Syria laidhinisha sheria
mpya za uchaguzi
Huku janga hilo la kibinadaamu
likiendelea,bunge la Syria leo limeidhinisha sheria mpya za uchaguzi ambazo kwa
mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mingi inaruhusu wagombea kadhaa
kuwania urais.
Sheria hiyo imeidhinishwa miezi
michache kabla ya uchaguzi mkuu.Hata hivyo sheria hiyo inawazuia viongozi wa
upinzani walio uhamishoni kugombea dhidi ya Assad kwani sheria hiyo inataka
wagombea wawe wameishi Syria kwa miaka kumi mfululizo.
Rais Assad anatarajiwa kugombea
muhula mwingine wa miaka saba.Uchaguzi sharti ufanywe kati siku sitni na tisini
kabla ya muhula wake kukamilika tarehe 17 mwezi Julai mwaka huu.
Upande wa upinzani na wapatanishi wa
kimataifa wamepinga kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu huku bado mazungumzo ya
kuvimaliza vita hivyo yakiwa bado yanaendelea.
Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa
na nchi za kiarabu kuhusu Syria Lakhdhar Brahimi akilihutubia baraza la usalama
la Umoja wa Mataifa jana amesema anahofia kuwa iwapo kutakuwa na
uchaguzi,upinzani hautakuwa na nia ya kufanya mazungumzo na serikali.
Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
Chanzo: Dwswahil.com
No comments:
Post a Comment