AZAM ina basi kali la kifahari,
uwanja wa maana na wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi nchini na
wanaoishi kitajiri zaidi lakini mastaa wake wametamka kwamba wana mchakamchaka
wa hatari ndani ya siku 18 kukata ngebe za Yanga.
Matajiri wametamka kwamba wana safari
ya siku 18 ambayo inaanza kesho Jumatano nje ya uwanja wao wa nyumbani kuusaka
ubingwa wa Ligi Kuu Bara, wanaamini kwamba wakishinda vita hiyo na kurejea Dar
es Salaam salama basi wana uhakika wa asilimia zote kuwa mabingwa wapya wa soka
nchini.
Azam imesaliwa na mechi tano tu
kumaliza ligi msimu huu lakini kati ya hizo mechi nne itacheza kwenye viwanja
vya ugenini wakati Yanga inayowakimbiza kwenye mbio za ubingwa ikiwa imesaliwa
na mechi mbili tu ugenini kati ya sita ilizonazo kumaliza msimu.
Safari hiyo ya siku 18 nje ya uwanja
wao wa Azam Complex itacheza mechi nne
mfululizo kabla ya kurejea uwanjani hapo Aprili 19 kucheza mechi yao ya mwisho
dhidi ya JKT Ruvu.
Matajiri hao wanaongoza ligi wakiwa
na pointi 47 kibindoni kesho watacheza na Mgambo JKT mjini Tanga ikiwa ni mechi
yake ya kwanza katika safari hiyo. Baada ya hapo itarejea Dar es Salam kucheza
na Simba kabla ya kurejea tena mikoani.
Azam inayosaka ubingwa Bara kwa mara
ya kwanza tangu iasisiwe mwaka 2007 itasafiri tena kwenda kucheza na Ruvu
Shooting mkoani Pwani Aprili 6 kabla ya kupaa kwenda Mbeya kucheza na Mbeya
City Aprili 13.
Safari hiyo itahitimishwa kwenye
mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu Aprili 19 kwenye uwanja wa Azam Complex.
Kocha msaidizi wa Azam, Ibrahim
Shikanda alisema kuwa licha ya timu yao kuwa na mechi nyingi ugenini bado wana
imani ya kufanya vizuri kwani timu yao imekua na historia nzuri katika mechi
ilizocheza ugenini kwa msimu huu.
Kiungo wa timu hiyo Salum Abubakar
‘Sure boy’ alisema, “Mechi za ugenini huwa zinakuwa ngumu lakini kwa kuwa
tumedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu ni lazima tujitahidi kushinda mechi zote
hizo.”
Naye mshambuliaji wa timu hiyo raia
wa Ivory Coast, Kipre Tchetche alisema: “Timu zinakamia sana kwa sasa hususani
zilizoko kwenye hatari ya kushuka daraja lakini kwa kuwa timu yetu ni kubwa na
inahitaji ubingwa ni lazima tupambane kuonyesha kuwa sisi ni bora.”
Azam itacheza mechi zake za ugenini
ikiwa na rekodi nzuri kwani katika mechi tisa ilizocheza ugenini imefungwa
mabao manne pekee ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja katika viwanja hivyo vya
ugenini.
Mshambuliaji wao, John Bocco alisema:
“Kazi kubwa tunayo wachezaji katika kipindi hiki kigumu ambacho ligi inaelekea
ukingoni kwa kila timu kupambana ili ichukue ubingwa na nyingine zisishuke
daraja, hivyo lazima tushinde mechi hizi zilizobaki tuchukue ubingwa.”
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment